MAMIA WAUPOKE MWILI WA TSVANGIRAI

Mamia ya raia nchini Zimbabwe, waliijitokeza katika uwanja mkuu wa ndege kuulaki mwili wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini humo Morgan Tsvangirai ulipokuwa unawasili kutokea nchi Afrika Kusini. Tsvangirai alifariki akiwa anapatiwa matibabu ya saratani, na mwili wake uliwasili hapo jana tayari kwa maziko nyumbani kwake. Tsvangirai aliyekuwa mpinzani mkubwa na asiliye na hofu dhidi ya chama tawala cha Zimbabwe ZANU-PF alikutwa na umauti akiwa na miaka 65, baada ya kuugua kwa muda mrefu saratani ya utumbo. Wafuasi na maafisa kutoka chama chake cha Movement for Democratic Change MDC, walikusanyika katika uwanja wa ndege wa Robert Mugabe, wakiimba nyimbo za maombolezo za Kikristo pamoja na za chama chake wakati ndege iliyobeba mwili wake ilipowasili. Mmoja wa manaibu wa Tsvangirai Nelson Chamisa alisema wameupokea mwili wa rais wao, shujaa wao na kiongozi wao. Mwili huo ulipelekwa katika kambi ya jeshi, ambako miili ya mashujaa wa kitaifa hupelekwa na wanachi kupata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kabla ya maziko. Atazikwa siku ya Jumanne kijijini kwake Buhera kilomita 250 kusini mwa mji mkuu Harare.

0 comments: