MKUTANO WA KWANZA SHAMBULIO LA MOYO WAFUNGWA JIJINI DAR ES SALAAM

 

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shakalaghe akimpa cheti cha kutambua umuhimu wake katika kutoa huduma za matibabu ya moyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu wakati wa kufunga mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza jijini Dar es Salaam

  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shakalaghe akimpa cheti cha kutambua umuhimu wake katika kutoa huduma za matibabu ya moyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kufunga mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza jijini Dar es Salaam.
  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shakalaghe akimsikiliza Afisa Mauzo kutoka kampuni ya usambazaji wa dawa ya SUN PHARMA Innocent Maro lipotembelea kuona huduma zinazotolewa na kampuni hiyo wakati wa kufunga mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza jijini Dar es Salaam
  Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Khuzeima Khanbhai akipokea cheti cha kushiriki kuandaa mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo ulioandaliwa na Taasisi hiyo na kumalizika jana jijini Dar es Salaam
  Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Engerasia Kifai akipokea cheti cha kushiriki kuandaa mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo ulioandaliwa na Taasisi hiyo na kumalizika jana jijini Dar es Salaam
  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya Computech Limited Sandip Datta akipokea cheti cha kutambua mchango wake katika kushirikiana na JKCI kufanikisha mkutano wa kwanza wa shambulio ya moyo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu Dkt. Seif Shakalaghe wakati wa kufunga mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza jijini Dar es Salaam.






Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya MOI. Dkt. Reuben Mutagaywa akipokea cheti cha kushiriki wakati wa kufunga mkutano wa Shambulio la moyo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza jijini Dar es Salaam.
 Mwandishi wa habari kutoka ITV Agnery Myala akipokea cheti cha kukitambua chombo cha habari cha ITV kwa kushirikiana na JKCI kufanya kipindi cha kutangaza kuhusu ugonjwa wa shambulio la moyo  wakati wa mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kumalizika jana jijini Dar es Salaam. Vyombo vingine vya habari vilivyopewa cheti kwa kushirikiana na JKCI kutangaza kuhusu shambulio la moyo ni pamoja na TBC, Channel 10, Star TV, Clouds TV, Azam TV na ZBC

 Baadhi ya washiriki wa mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa wakati wa mkutano kabla ya kufunga mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza jijini Dar es Salaam. (PICHA NA KHAMISI MUSSA NA JKCI)

Na Mwandishi wetu

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetakiwa kuendelea kufanya mikutano inayotoa mafunzo kwa wataalam wa afya itakayosaidia kuweka mbinu za kujikinga na magonjwa yasiyo ambukiza pamoja na kutafuta namna ya kutatua magonjwa hayo.


Rai hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shakalaghe wakati wa kufunga mkutano wa kwanza wa Shambulio la moyo uliofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Larger Plaza uliopo jijini Dar es Salaam.


Dkt. Shakalaghe alisema mkutano huo umekuwa wa faida kwa wataalam wa afya kwani sasa wataenda kuongeza jitihada za kuokoa maisha lakini pia kuwapa nafasi wananchi kutambua dalili za ugonjwa huo hivyo kuchukua hatua za haraka pale wanaposikia dalili za shambulio la moyo.


“Wizara ya Afya itahakikisha mikutano hii inafanyika kila mwaka kuwakusanya wataalam wa afya maeneo tofauti ya dunia ili kwa pamoja waweze kubadilishana ujuzi na kutatua tatizo la shambulio la moyo ambalo kwa sasa linaonekana kuongezeka”,


Akizungumza katika Mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo umewahusisha wataalam wa afya 300 kutoka nchi mbalimbali kujadili namna ya kuwahudumia wagonjwa wanaopata shambulio la moyo kwani sasa limekuwa tatizo kubwa katika jamii.


“Tatizo la shambulio la moyo linasababisha vifo vingi, wagonjwa wenye matatizo ya moyo duniani wanakaribia milioni 17 lakini wale wanaopata mstuko wa ghafla wa moyo ni karibu milioni sita duniani kote na kati yao asilimia 15 hupoteza maisha yao”, alisema Dkt. Kisenge


Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema shambulio la moyo hata hapa nchini lipo kutokana na mfumo wa maisha ya kila siku ikiwemo uvutaji wa sigara, kutofanya mazoezi, kula mlo usio na afya, kuwa na uzito uliopitiliza hivyo kupelekea matatizo ya moyo likiwemo shambulio la moyo.


“Mkutano huu umewakutanisha wataalam wa afya ili kuona ni kwa namna gani wataweza kuzuia tatizo la shambulio la moyo kwa kuwaelimisha wananchi kufika mapema hospitali kwasababu mtu akipatwa na shambulio la moyo anapaswa kufika hospitali mapema kwa ajili ya kupatiwa matibabu”,


“Tumeona tufanye mkutano huu uliowakutanisha wataalamu wa afya kutoka nchi za Marekani, Agentina, Misri, India, Sudani, Kenya, Tanzania na nchi nyinginezo kubadilishana ujuzi na kutengeneza mfumo wa kutambua matatizo ya moyo na kuwaelimisha wataalamu wengine ambao hawakupata nafasi kushiriki katika mkutano huu”, alisema Dkt. Kisenge


Dkt. Kisenge alisema dalili za mstuko wa moyo ni pamoja na kupata maumivu makali ya kifua yanayoenda hadi kwenye mkono na taya, kutokwa jasho jingi, kukosa nguvu na kushindwa kupumua vizuri hivyo kuwataka wananchi wanapopatwa na dalili hizo wafike kwa wataalam wa afya ili waweze kuchunguzwa na kupatiwa huduma kwa wakati.


Naye mshiriki wa mkutano huo Daktari bingwa wa magonjwa ya dharura na ajili kutoka hospitali ya KCMC Fransis Sakita aliipongeza JKCI kwa kufikiria kuandaa mkutano huo ambao ungepaswa kufanyika siku za nyuma kwani uhitaji wa taalama iliyotolewa katika mkutano huo ni hitaji kubwa kwa wataalam wa afya.


Dkt. Fransis alisema kwa upande wa KCMC asilimia 22 ya wagonjwa wa moyo waliowahi kuwaona walikuwa na tatizo la shambulio la moyo hivyo kuona kuna uhitaji mkubwa wa jamii kuufahamu vizuri ugonjwa huo ili waweze kujikinga.



“Katika Hospitali yetu mwanzo kulikuwa na uhaba wa vifaa vya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo lakini sasa hivi tumepata vifaa vya kutosha pamoja na elimu ya mara kwa mara hivyo kutuwezesha kutambua wagonjwa na kuwapatia huduma kwa wakati” alisema Fransis 

0 comments: