Latest Articles

OPERESHENI YA KULIPIZA KISIASA YA YEMEN YAUA ASKARI 7 WA SAUDIA

Operesheni ya kulipiza kisiasa ya Yemen yaua askari 7 wa Saudia
Walenga shabaha stadi wa jeshi la Yemen wameua kwa kuwafyatulia risasi wanajeshi saba wa Saudi Arabia katika maeneo ya Najran na Jizan, ikiwa ni radiamali kwa mashambulizi ya anga ya Riyadh dhidi ya nchi hiyo.
Duru za kijeshi nchini Yemen zimesema walenga shabaha hao wa jeshi la Yemen wakishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi walifanya operesheni hiyo jana Ijumaa, ambao askari watano wa Saudia waliuawa katika kijiji cha Hamezah katika eneo la Jizan, yapata kilomita 967 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Saudia, Riyadh.
Wanajeshi wengine wawili wa Saudia waliuawa jana alasiri kwa kumiminiwa risasi katika kambi ya jeshi ya Raqabat al-Zour, iliyoko katika eneo la Najran, umbali wa kilomita 844 kusini mwa Riyadh.
Sehemu ndogo ya hujuma za Saudia dhidi ya jirani yake Yemen
Mapema jana ndege za kivita za Saudia zilifanya mashambulizi matatu ya anga katika wilaya ya Razih, kaskazini mashariki mwa eneo la Sa'ada. 
Saudi Arabia na washirika wake waliivamia Yemen tangu mwezi Machi mwaka 2015 na hadi sasa nchi hizo zinaendelea kuizingira nchi hiyo kutokea nchi kavu, majini na angani na zimeua raia wasio na hatia zaidi ya 13,000 na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. 
read more

TRUMP, ADUI WA HAKI ZA BINADAMU DUNIANI

Trump, adui wa haki za binadamu duniani
Katika kukaribia mwaka wa pili wa Rais Donald Trump kuwa ofisini, mashirika ya haki za binadamu yamekosoa vikali utendaji wa serikali ya Marekani na hasa Trump mwenyewe kwa kuvunja haki za binadamu.
Akizungumzia suala hilo hivi karibuni, Kenneth Roth, mkurugeni mwandamizi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lililo na makao makuu yake mjini New York Marekani, ameutaja utendaji wa Trump kuhusiana na suala zima la haki za binadamu kuwa janga kubwa na kusema rais huyo ni dikteta anayeunga mkono tawala zisizo za kidemokrasia kama Saudi Arabia. Wakati huohuo maripota wasio na mipaka wametoa taarifa wakiashiria matamshi ya hujuma na dharau ya Trump dhidi ya vyombo vya habari na kusema kuwa tabia yake hiyo ni tishio kubwa kwa demokrasia ya Marekani. Zeid bin Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Biandamu wa Umoja wa Mataifa pia amesema kuwa Donald Trump anatishia uhuru wa vyombo vya habari nchini humo.
Kenneth Roth, Mkurugezi Mwandamizi wa Human Rights Watch
Hata hivyo ni wazi kuwa suala la ukiukaji wa haki za binadamu halihusiani tu na Rais Trump bali kwa miongo kadhaa sasa marais wa Marekani wamekuwa wakikiuka wazi haki za binadamu ndani na nje ya mipaka ya nchi hiyo. Kwa mfano katika utawala wa George W. Bush, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulifanyika ndani na nje ya nchi hiyo kukiwepo kuanzishwa jela za mateso na za kuogofya za Guantanamo nchini Cuba na Abu Ghurain huko Iraq na vilevile kuteswa wafungwa kwa kuzamishwa majini. Katika kipindi cha Barack Obama pia, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulifanywa na askari jeshi wa nchi hiyo katika pembe tofauti za dunia na hasa nchini Afghanistan ambapo ndege za kijeshi zisizo na rubani za Marekani zilitumika kuua maelfu ya raia wasio na hatia. Hii ni katika hali ambayo uungaji mkono wa Marekani kwa nchi na tawala nyingine zinazokiuka wazi haki za binadamu kama Saudi Arabia, Bahrain na utawala haramu wa Israel umekuwa ukiendelea kwa miaka hii yote.
Sehemu ya maafa na uharibifu unaofanywa na Saudia nchini Yemen
Pamoja na hayo lakini vitendo na matamshi ya Trump dhidi haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari yameufikisha ukiukaji huo wa haki za binadamu katika hatua nyingine hatari. Trump anachukuliwa kuwa ni mtu aliye na chuki kali dhidi ya wahajiri, wageni na Waislamu na asiyesita kutumia matusi dhidi ya binadamu wenzake. Ni hivi majuzi tu ambapo Trump aliwataja Wamexico kuwa watenda jinai, Waislamu kuwa magaidi na Waafrika kuwa shimo la choo. Ushindi wake chini Marekani hivi sasa umeyapa nguvu mpya makundi yenye misimamo ya kupindukia mipaka, ya kibaguzi na yenye chuki kali na yanayotumia mabavu dhidi ya wenzao ndani na nje ya mipaka ya Marekani, makundi ambayo huwa hayasiti hata kidogo kutenda jinai na kukiuka haki za binadamu pamoja na uhuru wa watu binafsi na wa kiraia.
Kuhusu siasa za nje pia, hatua ya Trump ya kuichagua Saudia kuwa nchi ya kwanza aliyoitembelea akiwa Rais wa Marekani, nchi ambayo iko mstari wa mbele wa kukiuka haki za binadamu na inayohusika moja kwa moja katika mauaji ya Waislamu katika vita vyake vya kivamizi huko Yemen, inaonyesha ni kwa kiwango gani Marekani haijali kuhusu suala la kuheshimiwa haki za binadamu.
Ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Wazayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia
Trump pia ameyakasirisha mno mashirika mashuhuri ya kutetea haki za binadamu kutokana na hatua yake ya kuunga mkono kuendelea kujengwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina pamoja na uamuzi wake wa hivi karibuni wa kutambua rasmi mji mtakatifu wa Quds eti kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Pamoja na hayo, lakini haionekani kuwa malalamiko na ukosoaji huo wote wa mashirika na taasisi za kimataifa utamfanya Donald Trump ambaye ameipa kipaumbele nara ya 'Marekani Kwanza' katika siasa zake kulegeza msimamo na kuheshimu haki za binadamu pamoja na uhuru wa kujieleza wa vyombo vya habari.
read more

SAKATA LA MELI ZINAZOBEBA MIHADARATI ZIKIWA NA BENDERA YA TANZANIA, LAMLAZIMU RAIS MAGURULI KUSITISHA USAJILI WA MELI

Sakata la meli zinazobeba mihadarati zikiwa na bendera ya TZ, lamlazimu Rais Magufuli kusitisha usajili wa meli
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania ameagiza kusitishwa mara moja usajili wa meli mpya nchini humo kufuatia kukamatwa dawa za kulevya na bidhaa nyingine zilizopigwa marufuku kimataifa ndani ya meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume kufuatilia suala hilo mara moja. Kadhalika Magufuli amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga kusimamia utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha kuwa jina la Tanzania halichafuliwi ndani na nje ya nchi.
Moja ya meli zenye bendera ya Tanzania
“Kafanyeni uchunguzi wa kina kwa meli zote zinazopeperusha bendera ya Tanzania, fanyeni uchunguzi kwa meli zilizokamatwa ambazo ni tano na pia hizi 470 zilizosajiliwa na zinaendelea kufanya kazi zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu lichafuliwe na watu wanaofanya mambo kwa masilahi yao.” Amesema Rais Magufuli. Kadhalika amehimiza kutekelezwa kwa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais Bi Samia Suluhu Hassan juzi, ambaye alitangaza kuzifutia usajili meli mbili zilizokamatwa hivi karibuni sanjari na kuamuliwa kushushwa bendera ya Tanzania kwenye meli hizo.
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania
Suluhu alizitaja meli hizo kuwa ni Kaluba iliyokamatwa maeneo ya Jamhuri ya Dominican Desemba 27 mwaka jana ikiwa na wastani wa tani 1.6 ya dawa za kulevya pamoja na Andromeda ambayo nayo iliyokamatwa ikisafirisha silaha kinyume cha sheria za kimataifa. Matukio ya kukamatwa meli zenye mihadarati na zinazopeperusha bendera ya Tanzania, yamekuwa yakiripotiwa nchi tofauti za dunia.
read more

MBUNGE WA MBEYA JOSEPH MBILINYI 'SUGU', AMENYIMWA DHAMANA TENA NA AMERUDISHWA RUMANDE HADI 22 JANUARI 2018


DT5P4SHWsAE1cVc.jpg
Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Joseph Mbilinyi “Sugu’’ pamoja na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Emmanuel Masonga, wamerudishwa rumande hadi Jumatatu ijayo ambapo kesi yao ya kutoa matamshi ya uchochezi itaanza kusikilizwa mfululizo.

Wawili hao, walifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza Jumanne tarehe 16 Januari, 2018 katika Mahakama ya Mkoa wa Mbeya na mahakama iliwanyima dhamana na kuamuru wapelekwe rumande mpaka tarehe 19 Januari 2018(leo) ambapo pia wamenyimwa dhamana hadi Jumatatu.

Kesi hiyo ambayo watuhumiwa wanasimamiwa na Wakili msomi Boniface Mwabukusi ilifunguliwa kutokana na maneno waliyotoa katika hotuba zao walizotoa katika Mkutano wa Hadhara wa Mbunge huyo wa Mbeya Mjini uliofanyika tarehe 30 Disemba, 2017 katika kiwanja cha Shule ya msingi Mwenge iliyopo katika Kata ya Ruanda jijini Mbeya.

Mashtaka yao ni matumizi ya lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli ambaye amechaguliwa na Watanzania wakiwamo watu wa Mbeya

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya amesema sababu kumnyima dhamana mshtakiwa Sugu na mwenzake Emmanuel Masonga ni hofu ya mshtakiwa kutohudhuira mahakamani mara kwa mara.

read more

MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA WAZIRI MKUU MAJALIWA WILAYANI SERENGETI NA BUNDA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mfereji wa maji wakati alipozindua chama cha ushirika cha Igembe Sabo kinachojishughulisha na kilimo cha mpunga  wilayani Bunda Januari 19, 2018. (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi cheti cha shukurani, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengti, Bw. William Mwakileme kutokana na mchango mkubwa wa hifadhi hiyo katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Robada wilayani Serengeti. Mheshimiwa Majaliwa alikuwa katika ziara ya mkoa wa Mara Januari 19, 2017. Katikati ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mara, Samweli Kiboyi.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha  Hunyari baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi ya wazazi katika zahanati  hiyo wilayani Bunda.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. akikagua mashine za kusukuma maji wakati  alipoembelea mradi wa chanzo cha maji Bunda akiwa katika ziara ya mkoa wa Mara.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizindua ushirika wa Igembe Sabo wilayani Bunda akiwa katika ziara ya mkoa wa Mara.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwakabidhi  hati ya usajili wa chama viongozi  wa chama cha ushirika cha Igembe Sabo cha Bunda , Malongo Mashimo ambaye ni Katibu (kulia) na Maria Nengwa ambaye ni Mwenyekiti wa Ujenzi baada ya  kuzindua ushirika huo akiwa katika ziara ya mkoa wa Mara.
read more

RAIA 700,000 WA SUDAN KUSINI WALIKIMBIA NJAA, VITA, MAGONJWA MWAKA JANA

Raia 700,000 wa Sudan Kusini walikimbia njaa, vita, magonjwa mwaka jana
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema raia takriabani laki 7 wa Sudan Kusini walikimbilia nchi jirani kutokana na migogoro, njaa na magonjwa katika mwaka 2017.
Ofisi hiyo imesema watu milioni 4 wamekimbia makwao, wakiwemo wakimbizi milioni 1.9 wa ndani, na zaidi ya milioni 2 waliokimbilia nchi za jirani zikiwemo Uganda, Kenya, Ethiopia, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ofisi hiyo pia imesema idadi ya Wasudan Kusini walioikimbia nchi yao mwaka jana, imepungua kuliko watu laki 7.6 mwaka juzi.
Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza mwezi Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.
Rais Salva Kiir (kushoto) na kiongozi wa waasi Riek Machar
Mwezi uliopita wa Disemba, Serikali ya Sudan Kusini ilitiliana saini mapatano ya usitishaji vita na makundi ya waasi nchini humo katika jitihada za hivi karibuni kabisa za kumaliza vita vya ndani ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa muda wa miaka minne nchini humo. Hata hivyo mapatano hayo yanalegalega huku kila upanda ukiutuhumu mwinginei kuwa unayakiuka.
read more

RAIS WA UGANDA ATAFAKARI KUREJESHA HUKUMU YA KIFO

Rais wa Uganda atafakari kurejesha hukumu ya kifo
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema anatafakari kurejesha hukumu ya kifo nchini humo ili kukabiliana na wimbi kubwa la uhalifu nchini.
Katika ujumbe aliotuma katika akaunti yake ya Twitter, Rais Museveni amesema amekuwa akisita kutia saini kila hukumu ya kifo anayoletewa tokea mwaka 1999. Hukumu ya kifo ambayo ndio adhabu kali zaidi Uganda kwa wanaohusika na uhalifu kama vile mauaji, uhaini na kunajisi haijawahi kutekelezwa tangu mwaka 1999. Idara ya Magereza Uganda inasema hivi sasa kuna wafungwa 278 ambao wamehukumiwa kifo lakini Rais Museveni hajatia saini amri ya utekelezwaji wa hukumu hizo.
Rais Museveni amesema watu wanatumia vibaya moyo wake wa huruma na sasa wengine wanadhani wanaweza kutenda uhalifu bila kuadhibiwa. Amesema anatafakari kuhusu kubadili msimamo wake huo wa kutotia siani adhabu ya kifo.
Kitanzi
Katika nchi jirani ya Kenya pia, hukumu ya kifo iko katika sheria lakini marais wa nchi hiyo hawajatia saini amri ya utekelezwaji hukumu hiyo kwa miaka 30 sasa. Oktoba mwaka 2016 Rais Uhuru Kenyatta alitia saini amri ya kubatilisha hukumu ya kifo ya wanaume 2,655 na wanawake 92 na kuifanya iwe hukumu ya maisha jela. Wakosoaji wanasema kutotekelezwa hukumu ya kifo kumepelekea kuongezeka kesi za uhalifu katika nchi hizo.
read more