AGENDA YA KUTOKOMEZA MALARIA IWE YA KUDUMU KATIKA VIKAO VYA MAAMUZI

 Na WAF, TABORA


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameziasa Kamati za Ulinzi na Usalama nchini kuona umuhimu wakuifanya ajenda yakutokomeza Malaria iwe yakudumu kwenye vikao vya maamuzi.

Dkt. Mollel ameyasema hayo leo, Aprili 25, 2024 akiwa amemwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye kilele cha Siku ya Malaria Duniani iliyofanyika mkoani Tabora na kusema kuwa kama nchi imeendelea kupiga hatua katika vita hivyo ikilinganishwa na miaka zaidi ya ishini iliyopita ambapo maambuki na vifo vya Malaria vilikuwa kati ya asilimia 45 hadi 50.

Aidha Dkt. Mollel amesema azma ya Serikali ni kufikia asilimia 3.5 ifikapo 2025 na kuwa na ziro Malaria 2030 huku akisisitiza kwa kusema itafikiwa endapo juhudi za Makusudi zitafanywa kwa ushirikiano baina ya Serikali na wadau

"Leo tunazungumza asilimia 8.1 kama nchi lakini miaka ya 1998, tulikuwa na kiwango cha juu sana, hivyo ili tuweze kufikia adhma yakumaliza kabisa malaria ifikapo 2030 kila mmoja wetu anawajibu wakufanya" amesema Mollel.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI Samsoni Maella, amesema Utumiaji wa Mifumo ya GoTHOMIS na FFARS imekuwa chachu ya kukusanya takwimu sahihi kwa ajili ya ngazi ya maamuzi, hali iliyochangia kufanya maamuzi sahihi kutokana na kuwa na takwimu sahihi.

"Kama Ofisi ya Rais TAMISEMI, tumefanikiwa kuimarisha miundo mbinu ya Afya na Rasilimali watu mathalani miaka mitatu nyuma tulikuwa na Hospitali za Wilaya 77 leo hii tunazo 177 hizi zimechochea sana uimarishaji wa huduma” amesema Mahela.

Naye Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI Dkt. Hamis Kigwangala ametoa wito kwa serikali na wadau kuongeza afua za kutibu watoto Shuleni, pia wafike maeneo ya Migodi, Mashamba Makubwa na maeneo ya Wafugaji.

Awali Msimamizi wa Miradi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim, akiwa amemwakilisha Katibu Mkuu, amesema kuchaguliwa kwa mkoa wa Tabora kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Wiki ya Malaria, ni pamoja na kuongeza nguvu ya afua za kupambana na Malaria kutokana na Mkoa huo kuwa na Maambukizi ya juu ya Ugonjwa huo ya asilimia 23.4 kwa sasa kutoka asilimia 11.7 kwa mwaka 2011.

0 comments: