Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema leo Jumapili (18.02.2018) kuwa nchi yake itachukua hatua dhidi ya Iran,na sio tu washirika wake wa mashariki ya kati, akirudia kwamba Tehran ni kitisho kikubwa kwa dunia.
Akiuhutubia mkutano wa usalama mjini Munich kwa mara ya kwanza, Netanyahu amewataka maafisa wa Marekani na Ulaya waliokusanyika pamoja na wanadiplomasia kupambana na Iran haraka, akionesha ramani inayoonesha kile alichosema kuwa ni uwepo wa Iran unaoongezeka katika mashariki ya kati.
Amesema Iran inaongeza nguvu zake wakati muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria unakomboa maeneo kutoka kwa wanamgambo hao.
Himaya ya Iran
"Kitu cha kusikitisha ni kwamba wakati IS inapotea na Iran inachukua maeneo yake, inajaribu kujenga himaya inayoendelea ikizunguka eneo la mashariki ya kati kutoka kusini nchini Yemen lakini pia ikijaribu kujenga daraja la ardhini kutoka Iran kwenda Iraq , Syria , Lebanon na Gaza," Netanyahu alisema. "Hizi ni hatua za hatari kwa eneo letu."
Wakati huo huo msemaji wa waziri mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki, ameamua kutotilia maanani maneno ya waziri mkuu yanayobadilisha mtazamo wa Poland wa ushirika katika mauaji ya Wayahudi , Holocaust na kuwa ni madai ya "Wayahudi wakosaji" kwa kusema ni matamshi ya kukaribisha mjadala wa wazi juu ya uhalifu wa vita vikuu vya pili vya dunia dhidi ya Wayahudi.
Wanasiasa wa Israel wamemshutumu waziri mkuu wa Poland kwa chuki dhidi ya Wayahudi kufuatia matamshi yake hayo jana Jumamosi (17.02.2018) katika mkutano wa usalama mjini Munich, akifungua ukurasa mpya katika mzozo wa hasira kuhusiana na sheria mpya ya Poland inayopita marufuku baadhi ya hotuba za mauaji ya Holocaust.
0 comments: