KOREA KASKAZINI: TRUMP NI MFANYABIASHARA WA VITA NA MNYONYAJI WA AMANI DUNIANI

Korea Kaskazini: Trump ni mfanyabiashara wa vita na mnyongaji wa amani duaniani
Serikali ya Korea Kaskazini imejibu matamshi ya uhasama ya Rais Donald Trump wa Marekani kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kusema kuwa, Trump ni mfanyabiashara wa vita na mnyongaji wa amani duaniani.
Gazeti la serikali ya Korea Kaskazini la Rodong Sinmun limeandika kuwa, Pyongyang itaendelea kusimama imara kwa nguvu zake zote dhidi ya vitisho vya Washington. Taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari vya Korea Kaskazini imesema kuwa, serikali ya Marekani chini ya uongozi wa Rais Donald Trump inashadidisha mgogoro katika Peninsula ya Korea kwa lengo la kuimarisha soko la mauzo ya silaha zake kwa Korea Kusini na Japan.
Mgogoro kati ya Korea Kaskazini na Marekani
Hii ni katika hali ambayo, hadi sasa tayari serikali za Seoul na Tokyo zimetangaza mpango wao wa kununua silaza za kisasa za Marekani, ukiwemo mpango wa kununua ndege za kivita aina ya F-35 za Marekani. Kabla ya hapo pia, Trump alitangaza kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa Twitter akitoa idhini ya kuziuzia nchi hizo mbili (yaani Korea Kusini na Japan) silaha za kisasa kwa kile alichokisema kuwa ni kukabiliana na Korea Kaskazini. Mgogoro wa Peninsula ya Korea umeendelea kuongezeka kutokana na siasa za uhasama za Marekani kwa kushirikiana na washirika wake katika eneo hilo. Kwa mara kadhaa Pyongyang imekuwa ikisisitiza kujizatiti kwa silaha za nyuklia na makombora ya balestiki madamu Marekani itaendeleza mkondo wake wa vitisho na uhasama dhidi yake.
Urafiki mkubwa uliopo kati ya Marekani na Korea Kusini na Japan
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini amesema kuwa, Korea Kaskazini inalipa gharama kutokana na majaribio ya silaha zake za nyuklia na kurusha makombora ya balestiki. Kang Kyung-wha amesema kuwa, Pyongyang itaendelea kukabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi kutokana na vikwazo ilivyowekewa na kwamba hatua hiyo inatokana na kulipa gharama ya kile alichokisema kuwa ni kuchafua usalama wa eneo la Korea.
Ameongeza kwa kusema kuwa, baadhi ya nchi za Magharibi zimekusudia kushadidisha zaidi vikwazo vyao kwa Korea Kaskazini na kwamba suala la nchi hiyo limekuwa ni changamoto kubwa katika siasa na usalama za Korea Kusini. Aidha amesisitiza kuwa huwenda vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini vikaendelea kuwepo kwa miaka mingi zaidi.

0 comments: