SIKU YA YOGA KIMATAIFA YAFANYIKA DAR,WIZARA KUJA NA PROGRAMU MAALUM KUHAMASISHA MAZOEZI

Na Mwandishi wetu, Michuzi TV


SIKU ya Kimataifa ya Yoga imefanyika nchini Tanzania kwa mwaka wa awamu ya 10(miaka 10) ambapo maelfu ya wananchi wakiwemo wenye asili ya India wameshiriki siku hiyo ambayo kwa Dar es Salaam imefanyika Viwanja vya Gymkana.

Mgeni rasmi katika Siku ya Yoga Kimataifa alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Gerson Msigwa ambaye ametumia nafasi hiyo kuhimiza Watanzania kufanya mazoezi ili kuweka afya zao vizuri.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa mazoezi ya Yoga ikiwa ni sehemu ya kuadhimimisha Siku ya Yoga Kimataifa,Msigwa amesema Wizara ya
Utamaduni, Sanaa na Michezo inaandaa programu ya viungo kwa kuwa na Michezo mbalimbali na Yoga ni miongoni mwa michezo itakayopewa kipaumbele ili wengi waweze kushiriki.

"Kwasasa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo tumeamua kuwashirikisha na Wizara ya Afya kuandaa programu maalum kwa ajili ya michezo mbalimbali ili Watanzania kote nchini wawe wanashiriki.Programu hii ya mazoezi ya viungo itakapokamilika tutautangazia umma wa Watanzania,tunataka watu wawe wanafanya mazoezi,"amesema Msigwa.

Amewaomba Watanzania kuwa Wizara itakapokuja na programu hiyo wawaunge mkono ili kujenga tabia ya kila mmoja kufanya mazoezi kama sehemu ya kuufanya mwili kuwa na afya nzuri na kuepuka na magonjwa yasiyoyakumbukiza ambayo mengi yanatokana na mtindo wa maisha ukiwemo wa kutofanya mazoezi.

" Tukija na hiyo program naomba watanzania tuunge mkono tujenge tabia ya kufanya mazoezi.Kwakufanya mazoezi kutawezesha kuwa na afya bora pamoja na kupunguza maradhi.Tuepuke vidonge na kwenda kwa waganga, tufanye mazoezi ili tuwe na afya nje. Ukiwa na afya nzuri utajenga uchumi wa taifa na familia," alisema.

Msigwa amesisi Yoga ni sehemu ya mazoezi ambayo ni muhimu ya kuujenga mwili vizuri, hivyo alishauri watanzania kujifunza Yoga iwasaidie kwa afya.

Kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na India amesema katika sekta ya Utamaduni,Sanaa na Michezo kumekuwa na ushirikiano mkubwa baina ya nchi hizo na kumekuwepo na mikataba kadhaa ambayo imeingiwa kwa lengo la kuendeleza sekta hiyo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Balozi wa India nchini, Manor Verma amesema kwamba Maadhimisho hayo ya Siku ya Yoga Kimataifa ni ya 10 kuadhimishwa kila Juni 21 ya kila mwaka ulimwengu.

Ameongeza kuwa watanzania wengi wameungana na India kueneza ujumbe wa Yoga na kwamba kauli mbiu ya mwaka huu inasema Yoga kwa ajili ya mtu binafsi na jamii nzima.

Amesema kuwa mazoezi ya Yoga yanahusisha namna ya kupumua, mazoezi ya shingo, mikono na viungo pamoja na tafakari huku akisisitiza Yoga imekuwa maarufu katika mataifa mbalimbali ulimwenguni kote na kwa Tanzania mbali ya Dar es Salaam pia imefanyika katika mikoa mingine nchini na watu 5000 wameshiriki.

0 comments: