RCHMT, CHMT SIMAMIENI MIRADI YA AFYA IKAMILIKE KWA WAKATI

  Na Mwandishi wetu Arusha


Timu za Usimamizi na Uratibu wa shughuli za afya ,Lishe, na Ustawi wa Jamii ngazi ya Mkoa (RCHMT) na Halmashauri (CHMT) zimetakiwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa miradi ya afya viporo ikamilike kwa wakati ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume ametoa kauli hiyo leo Februari 26, 2024 jijini Arusha alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya ya Afya na kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na Halmashauri ya Jiji la Arusha mkoani Arusha.

Dkt Mfaume amesema kuna baadhi ya maeneo miradi ya afya inasuasua na mingine haijakamilika na kuzielekeza timu hizo kuhakikisha inakamilika na kuanza kutoa huduma kwa jamii.

"Tusingependa kuona miradi imefikia asilimia 80 hadi 95 kuendelea kubaki hivyo na haikamiliki,hii haivumiliki hakikisheni inakamilika, RCHMT na CHMT ni jukumu lenu la msingi la kuhakikisha mnasimamia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yenu,hivyo hatutasita kuwachukulia hatua wale wote watakaolegalega katika suala hili,"amesema.

Amesema serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa, vifaa tiba pamoja na dawa hivyo ni wajibu wao kusimamia vituo vyote vya kutolea huduma vianze kufanya kazi.

Vilevile, ametaja mafanikio mengine ni kuajiri watumishi wa kada ya afya 17,000 na katika mwaka wa fedha 2023/24 tayari wameomba kibali cha kuajiri watumishi zaidi ya 10,305 na kuwataka viongozi hao kusimamia nidhamu kwa watumishi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

0 comments: