WAZIRI MCHENGERWA: 'SAMIA BOND' KUWASAIDIA WAKANDARASI WAZAWA

 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa ameelekeza TARURA kuanzisha mchakato wa upatikanaji wa hati fungani ya miundombinu ya Barabara (TARURA Infrastructure Bond) ambayo itaitwa ‘Samia Bond’ kwa kushirikiana na taasisi za kifedha nchini.


Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo Januari 24, 2024 kwenye kikao kazi chake na Menejimenti ya TARURA, Makatibu Tawala Wasaidizi (Miundombinu), Makandarasi Wazawa,Wataalamu Washauri na Taasisi za Kibenki kilichofanyika leo tarehe 24.12.2024 kwenye ukumbi wa kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Mwl.Nyerere (JNICC )jijini Dar es Salaam.

Waziri Mchengerwa amesema lengo la kuanzishwa kwa hati fungani hiyo ni kuwasaidia Makandarasi Wazawa kukabiliana na changamoto za kifedha wanazokumbana nazo na kuwawezesha kupata kazi za miradi mikubwa na waweze kuikamilisha kwa ufanisi.

“Matarajio yangu ni kuwa, hati fungani hii italeta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya miundombinu ya Barabara inayojengwa na TARURA na itaendana na kasi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwashirikisha na kufanya kazi na sekta binafsi, katika kutatua na kubuni mbinu za kuchochea gurudumu la kuwafikishia maendeleo wananchi”

Waziri Mchengerwa amesema kwenye eneo muhimu la matengenezo ya barabara, fedha hupatikana kutokana na makusanyo ya kila mwezi hivyo matengenezo hutegemea kupatikana kwa fedha baada ya makusanyo; Hali hii wakati mwingine husababisha matengenezo kuchelewa tuangalie namna ya kupata fedha kwa wakati ili kuendeleza miundombinu yetu”.

“Tafiti mbalimbali za Benki ya Dunia zinaonesha kwamba kuna madhara makubwa kiuchumi pale kazi za matengenezo ya barabara zinaposubiri au kuahirishwa na

wameonesha kwamba ukiwekeza Dola Moja ya Kimarakeni kwenye matengenezo ya barabara zilizo katika hali nzuri sasa utaokoa Dola Nne hadi Kumi za Kimarekani kulinganisha na iwapo matengenezo hayo yangeahirishwa”.

Hata hivyo amesema ndoto yake ni kuwatengeneza Wakandarasi wazawa mabilionea ambao watafanya kazi bila kushikwa mkono na kuishi ndoto ya kumsaidia Rais Dkt. Samia.

Kikao kazi hicho kwa upande wa TAMISEMI Kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa OR TAMISEMI Mhe.Deo Ndejembi,Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Miundombinu Mhandisi Rogatius Mativila,Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff, wawakilishi wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya TAMISEMI pamoja na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini.

0 comments: