ZITTO KABWE: MUNGU ALIAMUA NIINGIE MAHABUSU ILI NIJIONEE MATESO WANAYOPATA WANANCHI WENZANGU TANZANIA

Zitto Kabwe: Mungu aliamua niingie mahabusu ili nijionee mateso wanayopata wananchi wenzangu Tanzania
Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini, magharibi mwa Tanzania kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe amesema kuwa, inawezekana Mungu aliamua yeye akamatwe jana na polisi na kisha apelekwe mahabusu ili aweze kushuhudia mateso wanayoyapata watu wanaozuiliwa korokoroni kinyume cha sheria.
Akizungumza baada ya kuachiliwa na polisi mkoani Morogoro alikokuwa amezuiliwa Zitto ameelezea kile alichokikuta katika mahabusu hizo na kusema, kuna watuhumiwa waliowekwa mahabusu kwa muda mrefu bila ya kupelekwa mahakamani, suala ambalo mbali na kukiuka sheria, pia linawafanya watu hao kutojua mustakbali wao.
Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini
"Huko mahabusu nimekuta watuhumiwa wengi  ambao wengi wao wamekaa mahabusu bila ya kufunguliwa mashataka yoyote. Inawezekana Mungu ameamua niingie huko ili nijionee mateso wanayopata.” Amesema Zitto.
Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amekanusha madai ya mbunge huyo wa Kigoma Mjini magharibi mwa Tanzania juu ya kuwepo watuhumiwa wa muda mrefu katika kituo hicho akisema kuwa watuhumiwa wote hufikishwa mahakamani kwa wakati.
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei 
Matei ameyasema hayo ikiwa ni saa chache baada ya Zitto Kabwe kuachiliwa huru kwa dhamana na kuongeza kwamba, polisi ilimkamata na kumuweka mahabusu kwa kuwa alifanya mkutano wa hadhara bila ya kibali. Ameongeza kuwa, mbunge huyo anashtakiwa kwa vifungu 74 na 75 vya kanuni ya adhabu kwa kufanya mkutano bila ya kibali. Kamanda huyo amesema awali Zitto alikuwa akifanya mkutano wa ndani, lakini baadaye wananchi walijaa nje na ndipo alipotoka na kuwahutubia

0 comments: