MAKUMI YA WASICHANA WATOWEKA YOBO BAADA YA SHAMBULIZI LA BOKO HARAM

Makumi ya wasichana watoweka Yobo baada ya shambulizi la Boko Haram
Zaidi ya wasichana 90 wa shule wanahofiwa kutoweka baada ya kundi la kigaidi la Boko Haram kushambulia kijiji kimoja cha kaskazini mashariki mwa jimbo la Yobo nchini Nigeria.
Kutoweka kwa wasichana hao litakuwa miongoni mwa matukio makubwa ya aina hiyo tangu kundi la Boko Haram lilipoteka nyara wasichana 270 wa shule ya sekondari ya Chibok mwaka 2014. Tukio hilo lilielekeza macho ya walimwengu kwenye uasi wa karibu miaka 10 wa kundi hilo ambao Umoja wa Mataifa unautaja kuwa ni miongoni mwa migogoro mibaya zaidi duniani.
Baadhi ya watu wa eneo hilo wanasema waliwaona wasichana katika magari matatu aina ya Tata wakilia na kuomba msaada.
Polisi ya Nigeria na afisa mkuu wa elimu katika eneo hilo la Dapchi hawajathibitisha habari hiyo ingawa familia na watu walioshuhudia wanasema wasichana wengi wametoweka. Baadhi ya familia zimethibitisha kwamba watoto wao wa kike waliokuwa katika shule hiyo wametoweka.
Mamia ya wasichana wa shule ya Chibok walitekwa nyara
Watu walioshuhudia wamesema kuwa, wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram waliingia eneo la Dapchi Jumatatu iliyopita kwenye magari kadhaa wakiwa na bunduki. Waasi hao walifyatua risasi ovyo na kuwalazimisha baadhi ya wasichana na walimu wa shule ya eneo hilo kukimbia.
Zaidi ya watu elfu 20 wameuawa na mamilioni ya wengine kuwalazimika kuwa wakimbizi tangu kundi hilo la Boko Haram lilipoanzisha uasi nchini Nigeria mwaka 2009.

0 comments: