KUUAWA ASKARI WENGINE 12 WA IMARATI NCHINI YEMEN, MATOKEO YA KUPENDA KUJITANUA SAUDIA NA ABUDHABI


Kuuawa askari wengine 12 wa Imarati  nchini Yemen, matokeo ya kupenda kujitanua Saudia na Abu Dhabi
Wizara ya Ulinzi ya Yemen inayofungamana na Harakati ya Wananchi ya Answarullah, imetangaza habari ya kuangamizwa askari wengine 12 wa Imarati katika mji wa Taiz ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Hadi sasa mji wa Taiz umekuwa ukishuhudia mapigano na vita vya niaba. Kabla ya hapo pia yaani mwezi Novemba mwaka 2015 na Novemba 2017, mji huo ulishuhudia mapigano makali kati ya jeshi la Yemen kwa kushirikiana na Harakati ya Answarullah pamoja na wanamgambo wa Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kutoroka nchi kupitia vita vya muungano wa Saudia dhidi ya nchi hiyo, na hivi sasa pia ndani ya mwezi huu wa Februari, Taiz kwa mara nyingine tena unashuhudia vita na mapigano. Chanzo cha mapigano na vita hivyo kinarejea kwenye nafasi ya kijografia uliyonayo mji wa Taiz huko kusini mwa mji mkuu wa Yemen Sana'a, mji ambao uko umbali wa kilometa 256 kutoka mji huo.


Watawala wa Saudia na Imarati wanaopenda kujitanua
Kwa ibara nyingine ni kwamba, Taiz unahesabiwa kuwa lango la kuingilia mji wa Sana’a na kwa ajili hiyo kudhibitiwa na wapinzani wa ndani na vibaraka wa Saudia, kunaweza kuwafanya vibaraka hao kuingia mji mkuu huo wa Yemen ambao kwa sasa uko mikononi mwa harakati ya Answarullah na jeshi la taifa hilo. Hata kama nafasi ya Answarullah na jeshi la Yemen bado ni nzuri mjini Taiz, hata hivyo baadhi ya maeneo ya mkoa huo bado yako mikononi mwa askari wanaomuunga mkono Mansur Hadi, huku maeneo mengine yakiwa mkononi mwa magaidi wa kundi la ukufurishaji la al-Qaidah. Katika hali ambayo askari wa Saudia na Imarati kwa kushirikiana na askari wanaomuunga mkono Abdrabbuh Mansur Hadi na baadhi ya wapiganaji wa kikabila wamefanya juhudi kubwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwa ajili ya kuishinda harakati ya Answarullah na jeshi la Yemen, lakini juhudi hizo zimekuwa zikigonga mwamba.


Mashambulizi ya kutisha yanayofanywa na Saudia na Imarati nchini Yemen
Katika matukio ya hivi karibuni zaidi yanayohusiana na mkoa huo, ni kuangamizwa askari 12 wa Imarati sambamba na kujeruhiwa wengine kadhaa na hivyo kwa mara nyingine kuifanya Abu Dhabi inayopenda kujitanua ipate hasara kubwa nchini humo. Moja ya sababu za hasara hiyo, ni kupenda kujitanua na nafasi haribifu ya Imarati nchini Yemen. Weledi wa masuala ya Mashariki ya Kati wanazungumzia nafasi hiyo haribifu ya Imarati nchini Yemen kwa kusema: “Nafasi hiyo haribifu inatekelezwa kwa kuzua mapigano ya ndani kati ya makundi tofauti sambamba na kutuma fedha na silaha moja kwa moja kwa makundi hayo vibaraka na kadhalika kujenga jela za kutisha, kuendesha mauaji ya kuvizia na kushirikiana na wanachama wa kundi la kigaidi la al-Qaidah nchini humo. Lengo kuu la njama zote hizo ni kuweza kupora utajiri wa mafuta na gesi pamoja na vyanzo vingine huko kusini mwa Yemen na kadhalika kudhibiti baadhi ya maeneo yake ya kistratijia kama vile kisiwa cha Socotra.” Mwisho wa kunukuu.


Watawala wa Saudia wanafurahia mauaji ya raia wa Yemen
Sababu nyingine iliyopelekea Imarati kupata hasara kubwa nchini Yemen, ni mwendelezo wa siasa chafu za Abu Dhabi na Riyadh katika nchi hiyo. Hata kama Saudia na Imarati zimeingia katika tofauti kubwa baina yao kuhusiana na masuala mengi ya Yemen huku zikipata hasara kubwa za kijeshi, lakini inaonekana kwamba Abu Dhabu na Riyadh bado zinaendelea kushirikiana mjini Taiz. Katika uwanja huo Hamid Rizk, mtaalamu wa masuala ya Yemen anasema: “Hivi sasa Masalafi wa Kiwahabi walio mjini Taiz na wanaoungwa mkono na Imarati, wanakabiliwa na mashinikizo makubwa. Kushindwa Saudia na Imarati kufikia malengo yao katika vita dhidi ya Yemen, kumepelekea nchi mbili hizo kufumbia macho tofauti zao kuhusiana na baadhi ya maeneo ya Yemen ukiwemo pia mji wa Taiz na hivyo kuwawekea mipaka vibaraka wao hao.” Mwisho wa kunukuu. Ama nukta muhimu ya kumalizia ni hii kwamba, kuendelea kujitanua Abu Dhabi na Riyadh katika mgogoro wa Yemen, kunaweza kuzisababishia nchi hizo hasara kubwa isiyofidika nchini humo.

0 comments: