Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ametoa miezi mitatu kwa uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA kukamilisha malipo ya fidia ya shilingi milioni 771.6 kwa kaya 308 za Kitongoji cha Machimbo ili ziweze kupisha eneo la hifadhi katika Pori la Akiba la Mpanga Kipengele.
HASUNGA ATOA MIEZI MITATU WANANCHI WALIPWE FIDIA WAPISHE ENEO LA HIFADHI
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 10:41 AMNaibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ametoa miezi mitatu kwa uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA kukamilisha malipo ya fidia ya shilingi milioni 771.6 kwa kaya 308 za Kitongoji cha Machimbo ili ziweze kupisha eneo la hifadhi katika Pori la Akiba la Mpanga Kipengele.
Naibu Waziri Hasunga ametoa agizo hilo
jana katika mkutano wa hadhara baada kutembelea kitongoji hicho katika
Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wakati wa ziara yake ya kikazi kwa ajili
ya kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi mkoani humo.
“Kaimu Mkurugenzi (TAWA) kama unavyoona
wananchi hawa wapo tayari kupisha eneo hili la hifadhi, wanachosubiri ni
malipo yao ya fidia, naagiza mpaka ifikapo mwezi Februari mwakani
(2018) wawe wameshalipwa fidia zao, na ikiwezekana hata ndani ya mwezi
Januari wawe wameshalipwa,”alisema Hasunga.
Awali akiwasilisha taarifa ya pori hilo,
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, David Kenyata alisema wakati
pori hilo linaanzishwa mwaka 2002 kwa Tangazo la Serikali Na. 483
wananchi wa kitongoji hicho na vitongoji vingine walikuwa ndani ya eneo
hilo la hifadhi.
Alisema mazungumzo yalishafanywa kupitia
vikao halali vya uongozi wa viijiji na halmashauri ambapo wananchi hao
waliridhia kulipwa fidia ili kuachia maeneo hayo ya hifadhi.
Alisema sababu kubwa ya kuanzishwa kwa
pori hilo ni pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji yanayotiririka kwenda
mto Ruaha na kwenye mabwawa ya kidatu na mtera yanayotumika kuzalisha
umeme nchini.
Akizungumzia malipo ya fidia kwa vijiji
na vitongoji vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo alisema kijiji kimoja
kilishalipwa mwaka 2015 jumla ya shlingi milioni 500 na vijiji
vilivyosalia vitalipwa kwa awamu ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/2018
fedha zimetengwa kwa ajilia ya kulipa wananchi wa kitongaoji cha
Machimbo ambao tayari walishafanyiwa uthamini mwaka 2015.
Awali akizungumza na watumishi wa Pori
hilo katika ofisi zao zilizopo Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe,
Naibu Waziri Hasunga aliwataka watumishi hao kuongeza nguvu na ubunifu
kwenye kuzuia mifugo isiiingie hifadhini badala ya kusubiri iingie ndipo
waikamate na kuitoza faini au kuitaifisha.
“Nyie ni watalaamu, tumieni mbinu na
ubunifu wenu wote muhakikishe mnazuia mifugo isiingie hifadhini, sitaki
kusikia mmekamata au mmetaifisha mifugo hifadhini, hiyo siyo sifa, sifa
ni kuzuia isiingie kabisa, na nitawapima kwa hilo,” alisema Hasunga.
Aidha aliwataka watumishi hao kuimarisha
uhifadhi shirikishi, kujiepusha na vitendo vya rushwa, kufanya kazi kwa
kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuongeza ubunifu
utakaowezesha ongezeko la mapato ya Serikali.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo
aliwatembelea wananchi wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji
katika Skimu ya Igomelo ambao awali waligomea zoezi la uwekwaji wa
vigingi vya mpaka kwenye eneo lao na Pori la Akiba la Mpanga Kipengele
kwa hofu ya kupoteza maeneo hayo.
Hata hivyo baada ya kuwaelimisha kuwa
lengo la zoezi hilo ni kuiwezesha Serikali kufanya uamuzi wa mwisho wa
kumaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu baina ya vijiji na
maeneo ya hifadhi nchini wananchi hao walielewa na kuahidi kushirikiana
na mamlaka husika kukamilisha zoezi hilo kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Pori
hilo, Stanslaus Odhiambo alisema pori hilo linakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo uwepo wa vijiji na vitongoji 13 ndani ya pori hilo,
uchomaji moto maeneo ya hifadhi, ukataji miti hovyo, ujangili na uhaba
wa vitendea kazi.
Pori la Akiba la Mpanga Kipengele lina
ukubwa wa Kilometa za mraba 1574.25 katika wilaya ya Mbarali mkoani
Mbeya na Wilaya za Wanging’ombe na Makete Mkoani Njombe.
Na Hamza Temba, Mbarali – Mbeya
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Japhet Hasunga (waliokaa mbele katikati) akizungumza na watumishi wa
Pori la Akiba Mpanga Kipengele alipotembelea makao makuu ya pori hilo
jana katika Wilaya ya Wangin’ombe mkoani Njombe.
Baadhi ya watumishi wa Pori la Akiba Mpanga Kipengele wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (hayuko pichani).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Japhet Hasunga (wa pili kushoto) akisalimiana na Kaimu Meneja wa Pori la
Akiba la Mpanga Kipengele, Stanslaus Odhiambo muda mfupi baada ya
kuwasili makao makuu ya pori hilo jana katika Wilaya ya Wanging’ombe
mkoani Njombe.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Japhet Hasunga akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Machimbo wapatao
kaya 308 katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya jana ambapo aliiagiza
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania kuwalipa fidia ya shilingi
milioni 771.6 kabla ya Februari, 2018 ili wapishe eneo la Hifadhi
katika Pori la Akiba la Mpanga Kipengele.
Baadhi ya wananchi wa kitongoji cha
Machimbo wapatao kaya 308 katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya
wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ambaye
aliwatembelea jana na kuagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania iwalipe fidia ya shilingi milioni 771.6 kabla ya Februari, 2018
ili wapishe eneo la Hifadhi katika Pori la Akiba la Mpanga Kipengele
alipowatembelea.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na wananchi wanaojishughulisha na
kilimo cha umwagiliaji katika Skimu ya Igomelo, wilaya ya Mbarali Mkoani
Mbeya ambao waligomea zoezi la uwekwaji wa vigingi vya mpaka kwenye
eneo lao na Pori la Akiba la Mpanga Kipengele kwa hofu ya kupoteza
maeneo hayo. Baada ya kuwaelimisha wananchi hao walikubali kutoa
ushirikiano kwa mamlaka husika ili kukamilisha zoezi hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: