CUF YAWAOMBA RADHI WANACHAMA WAKE WA JIMBO LA KINONDONI


Chama cha Wananchi (CUF) kimewaomba radhi wapiga kura wa Jimbo la Kinondoni kufuatia mbunge wa jimbo hilo Maulid Mtulia kujiuzulu Ubunge na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na Wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma CUF, Abdul Kambaya, amesema chama hicho kinaomba radhi kutokana na kuwaaminisha wapiga kura kwamba Mtulia ni mtu makini mwenye uwezo wa kusimamia Sera za CUF na maendeleo ya Kinondoni.
“CUF haikutarajia kuingia kwenye uchaguzi mdogo kwa jimbo la Kinondoni kabla ya uchaguzi wa 2020 labda kama ingetokea kifo. Tunaomba radhi kwa kuwa tunaamini katika kurudia uchaguzi zitatumika fedha za umma wakati kwa hali tuliyo nayo fedha hizo zingeweza kuelekezwa kwenye shughuli za miradi ya maendeleo. Sababu za Mtulia kujiudhuru ni za msingi kwake lakini kwa upande wetu tunaziona hazina mashiko,” amesema
Kambaya amesema CUF inajiandaa kushiriki katika uchaguzi wa marudio ili kutetea jimbo la Kinondoni na kwamba itahakikisha inateua Mgombea makini na muadilifu atakayeleta ushindi kwa chama hicho.
Na Regina Mkonde

0 comments: