Zikiwa zimepita siku kadhaa tangu yalipojiri
mapinduzi baridi ya kijeshi nchini Zimbabwe, wingu la mgogoro wa kisiasa
lingali limetanda ndani ya nchi hiyo huku hatima ya mgogoro wenyewe
ikibaki kuwa kitendawili.
Mgogoro wa kisiasa ulianza nchini Zimbabwe baada ya wapinzani
wa Rais Robert Mugabe kulalamikia sera za kiongozi huyo hususan
kuhusiana na uhuru wa kisiasa, kupambana na ufisadi na vilevile sera
zake za kiuchumi. Uzee wa Mugabe mwenye umri wa miaka 93 na suala la
atakayekuwa mrithi wake ni maudhui nyengine iliyozusha taharuki na
kuzidisha mvutano wa kisiasa katika wiki za hivi karibuni nchini humo.
Wapinzani walikuwa na wasiwasi juu ya njia isiyo ya kidemokrasia ambayo
inaonekana Mugabe ametaka kuitumia kwa ajili ya kuainisha mrithi wake wa
uongozi; na hasa kutokana na ushindani mkali ambao umekuwa ukiendelea
kushuhudiwa kati ya mke wa Mugabe Grace na aliyekuwa makamu wa kiongozi
huyo Emmerson Mnangagwa.
Wakati huohuo, wengi walikuwa wakitabiri kwamba Mnangagwa angekuwa
ndiye mrithi wa Rais Mugabe katika mustakabali wa siasa za Zimbabwe,
lakini siku kadhaa zilizopita, na katika hatua ambayo haikutarajiwa
Mugabe alimuuzulu makamu wake huyo kwa kile alichodai kwamba ni kutokuwa
na imani na utendaji wake na kutotekeleza majukumu yake ipasavyo. Hatua
hiyo ya Rais wa Zimbabwe ilizidi kuipa nguvu dhana iliyokuwepo kuhusu
mpango wa kumfanya mkewe Grace kuwa mrithi wa uongozi baada yake; na
hata vyama vingi vya siasa viliitathmini hatua hiyo ya Mugabe kuwa ni
uandaaji mazingira ya kumweka Bi Grace madarakani. Kufuatia kujitokeza
kwa hali hiyo, jeshi liliingilia kati kwa kutuma magari ya deraya katika
barabara za mji mkuu Harare, kuvishikilia vituo vya redio na
televisheni za taifa na kumweka Mugabe mwenyewe kwenye kizuizi cha
nyumbani.
Ijapokuwa jeshi limetangaza kuwa limechukua hatua hiyo kwa madhumuni
ya kuwachukulia hatua wale liliowataja kama "wahalifu" waliomzunguka
kiongozi huyo, ambao wamesababishia Zimbabwe madhara na hasara za
kiuchumi na kijamii, lakini baada ya kupita siku chache tu tangu
yalipojiri mapinduzi ya kijeshi inaonekana kuwa mgogoro wa kisiasa wa
nchi hiyo umeingia kwenye awamu mpya.
Hivi sasa yameanza kufanyika mashauriano ndani ya nchi na kieneo juu
ya suala hilo huku kukiwepo na dhana kadhaa ikiwemo ile inayofikiriwa na
wengi kwamba Emmerson Mnangagwa, makamu wa rais aliyeuzuliwa ndiye
atakayeshika hatamu za uongozi wa nchi. Kama hilo litajiri, bila ya
shaka changamoto za kisiasa zitaendelea kushuhudiwa nchini Zimbabwe kwa
sababu watu wengi wanamwona yeye kama mtu wa mkono wa kulia wa Mugabe na
anayeshabihiana naye sana kwa sifa na tabia za kiuongozi. Vyama vya
upinzani vinamtuhumu Mnangagwa kuwa alihusika katika ukandamizaji
uliofanyika nchini humo hususan wakati wa uchaguzi, pamoja na wizi na
uporaji wa utajiri wa taifa. Kwa hivyo inatabiriwa kwamba endapo
atashika hatamu za uongozi, hatokuwa na uungaji mkono wa wananchi, zaidi
ya kutawala kwa kutegemea nguvu za kijeshi.
Wilf Mbanga, mchambuzi wa masuala ya kisiasa analizungumzia suala
hilo kwa kusema: "ikiwa Mnangagwa atakuwa ndiye atayechaguliwa, hakuna
matumaini yoyote ya kutokea mabadiliko chanya nchini Zimbabwe".
Kwa upande mwengine, mbali na jeshi, zaidi ya makundi 100
yanayojumuisha jumuiya na asasi za kiraia pamoja na viongozi wanaopinga
serikali yametoa taarifa ya pamoja ya kumtaka Mugabe ang'atuke
madarakani kwa amani, lakini hadi sasa kiongozi huyo amekataa kuachia
madaraka na kukabidhi hatamu za uongozi. Kutokana na hali hiyo, baadhi
ya wachambuzi wanahisi kwamba baada ya mashauriano, kuna
uwezekano Mugabe akarejea tena madarakani kwa sharti la kubaki uongozini
hadi utakapofanyika uchaguzi mkuu ujao.
Inavyoonekana, wanachokingojea kwa matarajio wananchi wa Zimbabwe ni
kuandaliwa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa kidemokrasia
nchini humo. Matumaini yao ni kuona kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo
anaondoka madarakani, kunaundwa serikali ya mpito na hatimaye baada ya
miongo kadhaa, yanaandaliwa mazingira ya kufanyika uchaguzi katika anga
huru na ya utulivu kwa kushirikisha wagombea wa vyama tofauti vya siasa
vya nchi hiyo.../
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: