''SERIKALI HAITAKI WACHUNGUZI WA NJE" MBOWE



Freeman Mbowe amesema hayo leo Septemba 22, 2017 wakati akizungumza na waandishi wa habari kutolea ufafanuzi mambo mbalimbali kuhusu sakata la Tundu Lissu na matibabu yake pamoja na kuelezea baadhi ya kauli ambazo zimekuwa zikitoka upande wa serikali.

"Kamati Kuu yetu iliomba uchunguzi wa sakata la Tundu Lissu ufanywe na chombo ambacho pande zote mbili zinaimani nacho, lakini serikali haitaki na jana kwa bahati mbaya sana Jaji Mkuu akatoa kauli kwamba vyombo vya ndani havijashindwa kufanya uchunguzi, sina kusudio la kubishana na Jaji Mkuu lakini kama kiongozi mwandamizi wa CHADEMA nadiriki kusema 'suspect' wetu namba moja kwenye shambulio la Lissu ni vyombo vya ulinzi na usalama hilo nalisema bila kumung'unya maneno" alisema Freeman Mbowe " amesema Freeman Mbowe 

Mbowe ameendelea kufafanua sababu ya wao kuhitaji uchunguzi wa nje na kusema "hadi sisi kudai vyombo huru vya kiuchunguzi ni kutokana na madhira mbalimbali tumeyapata kwa muda mrefu kutokana vyombo vya ndani vya ulinzi na usalama havina msaada katika madhira yanayotupata"
.
Ameelezea zaidi kwa kusema; "Baada ya uchaguzi Mkuu 2015 Mwenyekiti wetu wa mkoa wa Geita Alphonce Mawazo alishambuliwa mchana kweupe na watu ambao wanajulikana lakini polisi haikuchukua hatua yoyote ya maana, walisema wanachunguza lakini hawakuchunguza maana hakuna aliyepelekwa mahakamani mwaka wa pili sasa toka amefariki, Ben Sanane msaidizi wangu amepotea huu mwaka wa pili hakuna hatua zinachukuliwa na vyombo vyetu" alisema Mbowe 

Kiongozi huyo wa CHADEMA amesema kuwa wameshafanya mawasiliano na vyombo mbalimbali vya kiuchunguzi kutoka Marekani, Ujerumani na kusema wapo tayari kuja kutoa msaada wa kiuchunguzi wa jambo hilo. 

"Hata sasa hivi tumezungumza na vyombo vya kiuchunguzi vya Marekani, Ujerumani vipo tayari kuja kutoa msaada lakini wanataka maombi kutoka serikalini, ruhusuni hao watu waje kufanya uchunguzi watoe ushahidi wao, msibaki kusema ni CHADEMA, sijui wenyewe kwa wenyewe ,ruhusuni watu wenye utalaam wao waje kuleta vielelezo hapa huo ndiyo msimamo wa CHADEMA" alisema Mbowe 

Mbali na hilo Mbowe alimtaka Jaji Mkuu wa Tanzania kutambua kuwa wao wanamuheshimu na kusema mambo ya uchunguzi hausiki nayo 

"Tunaomba Jaji Mkuu asubiri tu ila mambo ya uchunguzi ni mambo ya polisi, Jaji Mkuu wewe muhimili wako ni Mahakama lakini hili suala la uchunguzi waachie polisi tunakuheshimu sana hatutaki kugombana na wewe, ila unapaswa kutambua kuwa tunapoomba uchunguzi kutoka nje ina maana hatuna imani na vyombo vya ndani watu wetu wanapotea, wanapigwa risasi, wanauwawa lakini hatuoni hatua za maana zikifanyika" alisisitiza Mbowe

0 comments: