TAASISI ZA KISHERIA ZAKOSOA JINAI ZA UTAWALA WA KIZAYUNI NA NJAMA ZA KUFUNIKA JINAI HIZO

Utawala wa Kizayuni umemzuia Ripota wa Masuala ya Haki za Binadamu kuingia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch hivi karibuni lilitoa ripoti zinazokosoa jinai za utawala huo wa Kizayuni.
Omar Shakir Ripota wa Masuala ya Haki za Binadamu wa Shirika la Human Rights Watch (HRW) amesema kuwa utawala wa Kizayuni umekataa kumpatia viza ya kuingia huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Utawala huo siku kadhaa zilizopita pia uliuzuia ujumbe wa bunge la Ulaya  kuingia huko Ukanda wa Ghaza. Katika hali ambayo ukosoaji na malalamiko dhidi ya hatua za mabavu za utawala wa Kizayuni unazidi kuongezeka, kundi moja kwa jina la "Kundi Kazi linalojihusisha na Watoto na Mizozo ya Silaha" limeutaka Umoja wa Mataifa kulijumuisha jina la jeshi la Israel katika faharasa ya wakiukaji wa haki za watoto. Ombi la kutaka kujumuishwa jina la utawala wa Kizayuni katika orodha ya wakiukaji wa haki za watoto limetolewa huku mwaka 2015 pia kukitolewa ombi kama hilo na taasisi za kisheria za kimataifa zilizotaka kujumuishwa jina la utawala wa Kizayuni katika orodho hiyo. Hata hivyo ombi hilo halikutekelezwa kutokana na mashinikizo ya Marekani na utawala wa Kizayuni. 
Dr Omar Shakir Ripota wa HRW aliyezuiwa na Israel kuingia huko Palestina
Taasisi za kisheria za Magharibi kwa kawaida hunyamaza kimya na kutochukua hatua yoyote mbele ya jinai zinazofanywa na Israel; na kwa hali yoyote ile radiamali zinazoonyeshwa na taasisi hizo kwa jinai za utawala wa Kizayuni na ukwamishaji wake katika utendaji wa taasisi hizo zinapaswa kuzingatiwa. Ripoti nyingi zimewasilishwa katika miaka ya hivi karibuni zikionyesha wazi wazi miamala na vitendo visivyo vya kibinadamu na vya utumiaji mabavu vinavyotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya makundi ya kutetea haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Mataifa kufikia sasa haujaonyesha radiamali yoyote kali kwa hatua za Israel za kukiuka pakubwa haki za binadamu kukiwemo kuwavunjia heshima na kuamiliana kusikostahili na wawakilishi wa taasisi za kisheria. Vitendo visivyoweza kuhalalishwa vya Israel mkabala na makundi na wanaharakati wa haki za binadamu na kamati za kutafuta ukweli za Umoja wa Mataifa vinabainisha wazi kwamba hakuna msingi wowote wa kisheria unaoweza kuukabili utawala huo ulio dhidi ya ubinadamu. Utawala wa Kizayuni ambao unahofia kufichuliwa zaidi jinai zake ambazo zinaweza kufuatiliwa kimataifa, umekuwa ukikwamisha kwa njia mbalimbali utendaji wa wajumbe wa Umoja wa Mataifa na wa taasisi nyingine za kimataifa zinazofuatilia jinai za Israel huko Palestina; na wakati huo huo kuzizuia tume za uchunguzi na za kutafuta ukweli za kimataifa na maripota wa Umoja wa Mataifa kuingia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Hii ni katika hali ambayo katika kuendelezwa siasa za kukaa kimya Umoja wa Mataifa mbele ya jinai zinazofanywa kila uchao na utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina wasio na hatia, Ban Ki-moon, katibu mkuu wa umoja huo aliyemaliza muda wake alijizuia kuchukua hatua dhidi ya Israel kutokana na mashinikizo ya Magharibi, licha ya kutakiwa na jamii ya kimataifa kuliorodhesha jina la utawala wa Kizayuni katika orodha ya tawala zinazokiuka haki za watoto. Si kwa Israel pekee, bali  Umoja wa Mataifa hata umekuwa ukitekeleza siasa za kunyamaza kimya mbele ya jinai za nchi kama vile Saudi Arabia; na hivyo kuziandalia uwanja wa kuendeleza jinai zao za kukiuka haki za watoto. 
Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa UN aliyemaliza muda wake 
Itakumbukwa kuwa katibu mkuu huyo wa zamani aliliweka jina la Saudi Arabia katika faharasa ya wakiukaji wa haki za watoto kutokana na kutenda mauaji dhidi ya watoto wa Yemen na kisha baada ya muda mfupi akalitoa jina la nchi hiyo katika orodha hiyo baada ya kutishwa na Saudia kwamba ingekata misaada yake ya kifedha kwa umoja huo. Katika mazingira kama hayo utawala wa Kizayuni na Saudi Arabia zinapata kiburi cha kuendeleza kirahisi jinai zao dhidi ya watoto; suala ambalo limewapelekea walimwengu kuendelea kushuhudia katika karne ya ishirini na moja vitendo vya dhulma, ukatili na mabavu vya tawala hizo wauaji wa watoto. 

0 comments: