MWANAMKE WA MISRI MWENYE UZITO WA KILO 500 AFIKA MUMBAI KUTIBIWA

Mwanamke raia wa Misri mwenye uzito wa kilo 500 amewasili Mumbai nchini India, ambapo anatarajia kufanyiwa misururu ya upasuaji kupunguza uzito wake. Inaripotiwa kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 36 huenda ndiye mwanamke mwenye uzito mkubwa kabisa duniani. Alisafirishwa kwa ndege inayosafirisha mizigo. Eman Ahmed tayari anaugua kiharusi ambacho kimesababisha mkono na mguu wake wa kulia kupooza, hali ambayo imeathiri uwezo wake wa kuzungumza. Amelazwa katika hospitali ya Saifee ambako wadi maalum yenye milango mikubwa na kitanda imara vimeundwa kwa ajili yake. Atafanyiwa misururu ya majaribio kabla madaktari kumfanyia upasuaji kupunguza uzito wake. Madaktari wanasema wanaweza kuchukua muda wa miezi sita au zaidi. Kulingana na taarifa kwenye mtandao unaomfanyia kampeni ya matibabu, Ahmed anaugua ugonjwa wa kisukari aina ya pili, shinikizo la damu, ugonjwa wa mapafu na nyongo miongoni mwa mengine makali. Ilibidi kreni kutumika kumpandisha kwenye ndege na pia kumshusha kwenye ndege.

0 comments: