MANJI AACHIWA KWA DHAMANA

Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii

Baada ya kusota rumande kwa takribani siku saba, hatimae Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusufu Manji amepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya. 

Manji ambae pia ni Diwani wa Mbagala Kuu na mfanyabiashara maarufu ameshtakiwa chini ya kifungu cha sheria namba 17(1)(a) ya sheria ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya namba 5 ya mwaka 2015. 

Amesomewa mashtaka yake leo na karani wa mahakama hiyo, Sarah Mulokozi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha. 

Manji amekananusha kutumia dawa za kulevya na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kuweka dhamana ya milioni kumi na mdhamini mmoja ambaye nae ameweka kiasi hicho hicho cha dhamana 

Manji alifika mahakamani hapo saa nane kasoro nne na alipandishwa mahakamani majira ya saa tisa. Katibu wa klabu hiyo, Charles Boniphace Mkwasa ndiye aliyemuwekea dhamana Manji na kumfanya awe huru. 

Katika kesi hiyo Manji anatetewa na mawakili watatu waliokuwa wakiongozwa na wakili Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Jeremiah Mtobesya huku upande wa Jamuhuri ukiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa mashtaka, Oswald Tibabyekomya aliyekuwa akisaidiana na wakili wa serikali Shadrack Kimaro. 

Akisoma hati ya mashtaka, Mulokozi amesema kuwa, kati ya Februari 6 na 9 mwaka huu huko Upanga Sea View ndani ya Wilaya ya Ilala jijiini hapa, mshtakiwa alitumia dawa za kulevya aina ya Heroine (diacefyl Morphine).. 

Mara baada ya kutimiza masharti ya dhamana Manji aliondoka katika viwanja vya mahakama hiyo akiwa katika gari aina ya Hummer lenye namba za usajili T 670 BBX huku akisindikizwa na umati wa mashabiki wa Yanga.

0 comments: