TAASISI YA MOYO YAFANYA UPASUAJI WA KUZIBUA MISHIPA YA MOYO ILIYOZIBA KWA ASILIMIA 100 NA KUSHINDWA KABISA KUPITISHA DAMU
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 12:45 PM
Profesa Mohammed Janabi, Mkuu wa Taasisi hiyo
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
Madaktari Afrika kutoka nchini Marekani kwa mara ya kwanza wamefanya
upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization Procedure) kwa mgonjwa na
kuzibua mshipa wa Moyo uliokuwa imeziba kwa zaidi ya miezi mitatu (kwa
lugha ya kitaalamu Chronic Total Occlusion).
Upasuaji huo ambao unatumia mishipa ya damu ulichukuwa muda wa saa
moja kwa kuzibua mshipa mmoja wa damu ambao ulikuwa umeziba kwa asilimia
100 na kushindwa kupeleka damu upande wa kushoto wa moyo.
Kambi ya Madakari wa Afrika imeanza tarehe 23/1/2017 na
inatarajiwa kumalizika tarehe 29/1/2017. Hadi sasa jumla ya wagonjwa sita
wameshapatiwa huduma za matibabu ya moyo ambayo ni kuzibua mishipa ya moyo
iliyokuwa imeziba. Hali za wagonjwa zinaendelea vizuri na wanatarajiwa
kuruhusiwa siku yoyote kuanzia kesho.
Tangu kuanza kwa mwaka huu wagonjwa 29 wameshafanyiwa
upasuaji wa bila kufungua kifua kati ya wagonjwa hao 23 wamefanyiwa upasuaji
katika kambi za ndani na wagonjwa sita wamefanyiwa upasuaji katika kambi ya
Madaktari Afrika.
Taasisi inaendelea kuwaomba Madaktari wote nchini wenye
wagonjwa wao wa matatizo ya moyo wawatume wagonjwa hao katika Taasisi ya
Moyo ili waweze kupatiwa matibabu. Kwa mawasiliano zaidi wawasiliane na
Dkt. Peter Kisenge kwa namba 0713 236 502 na 022-2151379 ambaye
atawaelekeza utaratibu wa kuwatuma wagonjwa hao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: