DIWANI ALILIA WAJAWAZITO MWAMBAO MWA ZIWA TANGANYIKA

NA MAGRETH MAGOSSO, KIGOMA

DIWANI  wa Kata ya Mwamgongo,  kilichopo mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika  Wilaya ya Kigoma,  Kasimu Nyamkunga ametishia kuandaa mandamano  na kwenda katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Emanuel Maganga endapo changamoto ya wajawazito kwenye Zahanati ya Mwamgongo kuendelea kutumia tochi za simu  kuzalishwa  na ujenzi wa choo kilichoanguka kutopatiwa ufumbuzi  .
                                                                  
Akithibitisha kauli hiyo mbele ya Jamboleo wilayani humo juzi Nyamkunga alisema wakazi wa vijiji vya mwambao mwa ziwa Tanganyika wanakabiliwa na changamoto nyingi katika sekta ya afya, elimu, nishati ya umeme na usafiri duni wa mitumbwi huku zahanati hiyo ikikosa hata nishati ya solar ilihali inatoa huduma kwa zaidi ya vijiji sita.

“kitendo cha kutumia tochi ni janga kwa wajawazito, lakini utawala hawaguswi katika hilo na hata  bajeti ya mwaka huu haipo ajabu wanasisitiza usafi lakini wamesahau zahanati hiyo haina choo kimeanguka , diwani nikisema wanasema siasa ,wakati wataalamu ndio wanasiasa hawajui vipaumbele vya wananchi kwa kuwa wanapenda kukaa maofisini watajuaje kero zetu”

Alisema ukosefu wa nishati ya umeme katika zahanati hiyo ni kuhatarisha afya kwa watoa huduma na wapewa huduma na inapotokea mama mjamzito kufanyiwa upasuaji wa dharura hakuna speed boti ya kumsafirisha katika hospitali ya rufaa ya mkoa kwa kuwa fedha za mradi wa boti  sintofahamu .

Naye Diwani wa viti maalum Hidaya Kipwi alifafanua kuwa kuwa changamoto ya zahanati hiyo ni vifo kwa wajawazito na wagonjwa wengine lakini wajawazito hupata huduma ya kujifungua kwa kutumia  tochi ya simu,hakuna glovu za mikono kwa  wahudumu ,changamoto hiyo imejitokeza Juni 2016 hadi sasa ni tete.

Alishauri kurudishwa kwa nishati ya umeme wa solar na ujenzi wa wodi ya upasuaji wa dharura ili kuondoa vifo vitokanavyo na uzazi unaochangiwa na huduma finyu katika zahanati hiyo inayotoa huduma za afya kwa vijiji sita vya mwamabo mwa ziwa Tanganyika na kumkumbusha mkurugenzi na idara ya afya wafanyie matengenezo ya boti la zahanati hiyo ambayo gharama yake haizidi fedha sh.milioni 4.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya kigoma Enock Chobhaliko alishauri kutumia vyanzo vya fedha katika soko la kalinzi na mkongoro ambayo yana uwezo wa kuingiza fedha zaidi ya milioni 3 kwa mwezi ili kukarabati  boti hilo ili kuepusha vifo kwa wagonjwa wenye hitaji la upasuaji wa dharura.

Akijibia hilo Kaimu Mkurugenzi Shija Leylla alisema  haina haja ya kuandamisha wananchi lakini atafika katika kijiji hicho na kushuhudia uhalisia wa mambo na mwanzoni mwa wiki ya leo solar itawekwa ili,kuepusha matumizi ya tochi za simu katika utoaji huduma kwa wajawazito na sula la  choo na boti vitashughulikiwa.

0 comments: