SERIKALI HAIKO TAYARI KUONA KIWANDA KINAFUNGWA-NGUVILA


Na.Angela Sebastian ,Bukoba

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Kagera ,Toba Nguvila  amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan haiko tayari kuona kiwanda cha kusindika kahawa ya unga TANICA  kinafungwa kwa  kukosa mtaji, mali ghafi na uchakavu wa mitambo.

Ametoa ahadi hiyo leo baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo Manispaa ya Bukoba kusikiliza kero za wafanyakazi ambao wamemueleza kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni ukosefu wa mali ghafi na mtaji ambao ungewazesha  kumudu kuingia katika ushindani wa soko.

"Rais Samia  na serikali yake hawezi kufumbia macho kuona kiwanda  hiki kilichoanzishwa  na serikali kinakufa,tutakaa na bodi  kuangalia namna ya kuhakikisha kinaendelea kukuzalisha ili wafanyakazi msimpoteze kazi  kwa sababu ndicho tegemeo lenu na familia katika kujipatia kipato,"amesema Nguvila,

 Meneja wa kiwanda hicho Experiu Cyliro ameeleza kuwa ifikapo wakati wa msimu wa kununua kahawa hasa katika minada hujikuta hawana mtaji hali inayosababisha wanunue kahawa kidogo au kukosa ukilinganisha na mahitaji  na  wakati mwingine hununua kwa bei kubwa kutoka kwa wanunuzi walionunua kwa bei ya chini wakati wa msimu.

Pia amesema  mitambo ya kiwanda hicho ilifungwa mwaka 1963 imechakaa ingawa  baadhi wameendelea kuifanyia ukarabati na mingine inahitaji kununuliwa mipya  na kutolea mfano mtambo wa kuzalisha hewa ya kukausha kahawa ya unga (air heater) ambao unagharimu sh. Milioni 370.

Cyliro amesema hali hiyo , inachangia uzalishaji kushuka na uchumi wa wafanyakazi kuteteleka  ikiwemo mishahara kushuka  na hivyo wanaiomba serikali kuangalia namna ya kuwanusuru na changamoto hiyo


0 comments: