SERIKALI YA ZANZIBAR YAANZA MCHAKATO WA UJENZI VITUO VYA MAFUNZO YA AMALI

 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza mchakato wa ujenzi wa vituo  vya Mafunzo ya Amali vitakavyojengwa Unguja na Pemba ili kuwasaidia Wanafunzi watakaokosa sifa za kujiunga na Elimu ya juu kujiendeleza na kupata ujuzi mbali mbali.


Akihutubia katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 59 ya Elimu bila ya malipo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali imekusudia kujenga vituo vitano vya Mafunzo ya Amali sambamba na kujenga Chuo cha ubaharia katika eneo la Bait el Ras Zanzibar.


Mhe.Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt Hussen Ali Mwinyi inaendelea na hatua mbali mbali za upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika katika kujifunza na kufundishia, kuzindua mradi mkubwa wa kuimarisha ubora wa elimu ya lazima sambamba na  kuwajengea walimu mbinu na uwezo wa kusomeshea ili kupata matokeo bora na kuimarisha ufanisi wa kazi.


Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa miongoni mwa matunda ya mapinduzi ya mwaka 1964 ni kuondoa ubaguzi  na kuleta usawa katika upatikanaji wa elimu kwa wote bila ya kujali itikadi, rangi, kabila, dini na uwezo wa kiuchumi.


Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa kwa Mwaka wa fedha 2023- 2024 Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imejipanga kujenga Skuli ishirini na sita (26) za ghorofa kwa Unguja na Pemba ambazo zitatatua changamoto ya uhaba wa madarasa, msongamano wa wanafunzi hasa katika visiwa vidogo vidogo vya Tumbatu na Kojani Pemba ambazo zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu .


Pia Makamu wa Pili w Rais amewapongeza wananchi wa Zanzibar  kwa kuthamini juhudi zinazochukuliwa na serikali kwa kuanzisha ujenzi wa skuli na madarasa kwa kujitolea pamoja na kuanzisha miradi ambayo Serikali imechukua hatua ya kukamilisha ujenzi hio.


Mhe. Hemed amewataka Viongozi, Walimu na watendaji wa Wizara ya Elimu kulitumia vyema Tamasha la Elimu bila ya Malipo kwa kuibua na kuendeleza Vipaji mbali mbali vya Vijana na kutoa wito kwa Wazazi na Walezi kuendelea kuwaruhusu Wanafunzi kushiriki katika Michezo ili kuimarisha ufahamu wao katika mafunzo sambamba na kuwataka Wanafunzi kulinda na kuendeleza mila na silka za Wazanzibari.


Nae waziri wa elimu na mafunzo amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa ameeleza kuwa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imeipa kipaimbele sekta ya elimu kwa kutenga fedha nyingi ili wanafunzi wapate elimu bora kwenye mazingira mazuri.


Amesema wizara itahakikisha pamoja na kusimamia kila mtoto anapata elimu ya lazima bure na katika mazingira wezeshi pamoja na kuwataka wazazi, walezi, wanafunzi na walimu kuthamini juhudi hizo kwa kuongeza mashirikiano na kusoma kwa bidii ili kupata matokeo mazuri yatakayoakisi dhamira ya mapinduzi ya Zanzibar kufuta ujinga na dhuluma.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Ndg. Khamis Abdallah Said ameeleza kuwa Tamasha la elimu bila ya malipo limejumuisha michezo mbali mbali lengo ni kuibua vipaji kwa wanafunzi vitakavyowasaidia kuweza kujiajiri ndani na nje ya nchi.


Ameeleza kuwa Wizara ikiwa katika Maadhimisho haya ya Hamsini na Tisa (59) ya Elimu bila ya malipo imeendelea kupiga hatua katika kuboresha Sekta ya elimu nchini hasa kuzingatia vigezo vya kimataifa kwa kusimamia wastani wa walimu na wanafunzi kwenye madarasa  kwa kujenga skuli za kisasa za ghorofa pamoja na kuwawekea samani na vifaa vifaa vya kufundishia.


 (PICHA NA OMPR)

   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla leo tarehe 23 Septemba 2023 akihutubia katika kilele cha Maadhimisho ya miaka 59 ya Elimu bila ya Malipo katika Viwanja vya Chuo cha Mafuzno ya Amali Vitongoji Wilaya ya Chake Chake Pemba

   Baadhi ya Wanafunzi wakiwawakilisha wanafunzi wenzao wa Mikoa mitano ya Zanzibar katika kilele cha maadhimisho ya Miaka 59 ya Elimu bila ya malipo kiwanja cha Chuo cha Mafunzo ya Amali Vitongoji Wilaya ya Chake Chake Pemba

0 comments: