SYRIA YAITAKA UN KUCHUKUA HATUA YA WAUNGAJI MKONO UGAIDI

Syria yaitaka UN kuchukua hatua dhidi ya waungaji mkono ugaidi
Serikali ya Syria imeuandikia barua Umoja wa Mataifa ikizungumzia ongezeko la mauaji ya kigaidi yanayofanywa dhidi ya raia wa Damascus na vitongoji vyake na kuutaka umoja huo kuchukua hatua dhidi ya nchi zinazoyasaidia na kuyafadhili makundi ya kigaidi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetuma barua mbili kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la umoja huo masaa kadhaa baada ya makundi ya waasi yaliyoko eneo la Ghouta Mashariki kulenga mji mkuu wa nchi hiyo na vitongoji vyake kwa maroketi ambayo yameua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.
Barua hiyo imelaani mashambulizi hayo iliyoyataja kuwa ni jinai zinazofanywa kila siku na magaidi hao dhidi ya raia na kusisitiza kuwa, zaidi ya maroketi 1500 yamevurumishwa dhidi ya mji wa Damascus na viunga vyake katika kipindi cha wiki saba zilizopita.
Magaidi wanashambulia mji wa Damascus kwa maroketi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imewatuhumu maafisa wa baadhi ya nchi za Ulaya kuwa wanaunga mkono na kuwasaidia magaidi bila ya kuchukuliwa hatua yoyote.
Mji mkuu wa Syria umeshuhudia mashambulizi mengi katika wiki za hivi karibuni kutoka maeneo ya karibu yanayodhibitiwa makundi vya wanamgambo wanaoungwa mkono na kusaidiwa na baadhi ya nchi za Magharibi kama Marekani.

0 comments: