WAFANYAKAZI WAPYA WA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) WAPIGWA MSASA

  Mkurugenzi  Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza leo na wafanyakazi wapya 57 walioajiriwa katika Taasisi hiyo kuhusu umuhimu kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma.
Na Mwandishi Maalum
WAFANYAKAZI wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma na kuepuka vitendo vya rushwa.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Prof. Mohamed Janabi, wakati alipokuwa akuzungumza na  wafanyakazi  wapya 57 wa kada mbalimbali walioajiriwa hivi karibuni.
Alisema miongoni mwa wafanyakazi hao, wapo madaktari, maafisa uuguzi, wahasibu, maafisa  Tehama, wahudumu wa afya, wataalam wa maabara na maafisa ustawi wa jamii.
“Mtumishi wa umma lazima ufanye kazi kwa kuzingatia maadili na sheria za kazi ikiwa ni pamoja na  kufanya kazi kwa ufanisi, weledi na kuzingatia maadili ya taaluma yako.
“Humu ndani ya taasisi kazi yetu inahitaji nidhamu ya hali ya juu kwa sababu tukikosea hata kidogo maana yake tunapoteza maisha ya mtu.
“Ukipangiwa zamu zingatia, msipokee rushwa, kwani ni kitu hatari sana ukimuona mwenzio anajihusisha na vitendo hivyo hatua ya kwanza ni kumkemea na kumshauri kuacha mara moja,” amesisitiza
Amewataka wafanyakazi hao kuzingatia kuvaa mavazi yenye staha wakati wote hususan wale ambao watakuwa hawavai sare maalum za kazi.
“Hakikisheni mnawahi kazini, kama unaishi mbali jitahidi kuwahi mapema kutekeleza majukumu yenu,” amewasihi.
Prof Janabi hakusita kuwaeleza wafanyakazi hao baadhi ya changamoto zinazoikabili taasisi hiyo ikiwamo ufinyu wa nafasi.
“Ofisi tulizonazo ni chache, kwa kuanzia tutashirikiana hivyo hivyo hasa wale ambao si wataalamu wa afya,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa Taasisi hiyo, Ghati Chacha alisema kati ya wafanyakazi walioajiriwa 23 ni wanaume na 29 ni wanawake.
“Wameajiriwa JKCI baada ya kupatiwa kibali na Serikali kulikuwa na nafasi 57 zilizojazwa ni 56 na hadi sasa walioripoti kazini ni 52, wanne wameomba udhuru kwani wana dharura na hadi kufikia wiki ijayo tunatarajia nao watakuwa wameripoti kazini,” amesema.

  Baadhi ya Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na vitengo vya  Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi (hayupi pichani) wakati akinzungumza na wafanyakazi wapya 57 walioajiriwa katika Taasisi hiyo.

Afisa Tawala  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Joachim Asenga akiwaelekeza jinsi ya kujaza fomu watumishi wapya 57 wa Taasisi hiyo ambao wameajiriwa hivi karibuni.(PICHA NA JKCI)

0 comments: