ZUMA: AFRIKA KUSINI ITARUHUSU UTAIFISHAJI WA ARDHI BILA YA FIDIA

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema leo kuwa nchi hiyo itazifanyia marekebisho sheria zake ili kuruhusu utaifishaji wa ardhi bila ya kuwalipa fidia wamiliki wa ardhi hizo, katika kipindi hiki ambapo nchi hiyo inajaribu kuharakisha zoezi la kuwagawia tena ardhi raia weusi walio wengi wa nchi hiyo.
Itafahamika kuwa sehemu kubwa ya ardhi ya Afrika Kusini inamilikiwa na wazungu kwa zaidi ya miongo miwili baada ya kumalizika utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo (Apartheid). Rais Zuma amesema katika hotuba yake akiashiria sera za kilimo za serikali yake kuwa, wanahitaji kuchukua hatua madhubuti zitakazobadili uchumi wa nchi hiyo kwa haraka, likiwemo suala la umiliki wa ardhi.
Moja ya mashamba ya zabibu yanayomilikiwa na wazungu nchini Afrika Kusini 
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa msimamo huo mkali ulioonyeshwa na chama tawala ANC unajiri sambamba na miito iliyotolewa na chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters ambacho kimetaka kutaifishwa ardhi zinazomilikiwa na wazungu huko Afrika Kusini. Wachambuzi hao pia wanasema kuwa serikali ya Afrika Kusini imechukua hatua hiyo ili kuungwa mkono kisiasa chama tawala katika ngome za vijijini kabla ya kufanyika uchaguzi wa ndani ya chama mwezi Disemba mwaka huu.

0 comments: