LIWALI WA ISIS AANGAMIZWA MOSUL, IRAQ; MAGAIDI 13 WAUAWA NA KUJERUHIWA

Vikosi vya Kujitolea vya Wananchi wa Iraq, maarufu kwa jina la al Hashdu al Sha'abi vimetangaza habari ya kuangamizwa Liwali wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika wilaya ya Tal Afar, magharibi mwa mkoa wa Nainawa (Nineve).
Vikosi hivyo vimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, ndege za jeshi la Iraq baada ya kubadilishana taarifa za kiintelijensia na vikosi vya al Hashdu al Sha'abi vimefanya shambulizi la anga kwenye eneo alipokuwa amejificha 'Mustafa Yusuf' Liwali wa kundi la kigaidi la Daesh katika wilaya ya Tal Afar na kumuangamiza.
Habari nyingine kutoka nchini Iraq zinasema kuwa, brigedi ya 11 ya vikosi vya al Hashdu al Sha'abi  jana Jumatano viliangamiza magaidi sita na kuwajeruhi wengine saba kusini magharibi mwa wilaya ya Tal Afar. Mtandao wa habari wa Iraq Press umeripoti habari hiyo na kusema kuwa Brigedi ya 11 ya al Hashdu al Sha'abi  imeangamiza magaidi hao na kuwajeruhiwa wengine saba katika operesheni ya kusafisha kitongoji cha "Ain Talawi" cha kusini magharibi mwa wilaya ya Tel Afar, magharibi mwa mkoa wa Nainawa.
Askari wa vikosi vya al Hashd al Sha'abi vikipambana na magaidi wa Daesh (ISIS) nchini Iraq

Vikosi vya al Hashdu al Sha'abi  jana Jumatano vilianza hatua ya sita ya operesheni zake za kijeshi katika upande wa magharibi wa mkoa wa Nainawa, wa kaskazini mwa Iraq na kufanikiwa kukomboa vijiji kadhaa kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh.
Itakumbukwa kuwa, mwezi uliopita, eneo la mashariki mwa mji wa Mosul lilikombolewa kikamilifu kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh na hivi sasa raia waliolazimika kukimbia maeneo yao kutokana na jinai za magaidi hao wakufurishaji wanaendeleo kurejea kwenye maeneo yao, huko mashariki mwa Mosul.

0 comments: