BIASHARA YA SILAHA IMEFIKIA KIWANGO CHA JUU ZAIDI KUWAHI KUSHUHUDIWA KWA MIONGO KADHAA

Uuzaji silaha duniani umefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa huku nchi za Kiarabu za eneo la Mashariki ya Kati zikiwa miongoni mwa wanunuzi wakuu wa silaha hizo.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya mauzo ya silaha iliyotolewa leo na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (Sipri).
Ripoti hiyo imeeleza kuwa silaha nyingi zaidi ziliuzwa kati ya mwaka 2012 na 2016 kuliko kipindi kingine chochote kile cha miaka mitano tangu mwaka 1990.
Miongoni wa wanunuzi wakuu waliotajwa kwenye ripoti hiyo ni Saudi Arabia ambayo imejiingiza kwenye uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen. Saudia imetajwa kuwa mnunuzi mkubwa zaidi wa silaha duniani baada ya India.
Wakati India imenunua karibu silaha zake zote kutoka Russia, Saudia imenunua mifumo yake mikuu ya silaha na zana za kivita kutoka Marekani na Uingereza.
Pieter Wezeman (wa kwanza kulia)
Pieter Wezeman, mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita akthari ya nchi za Mashariki ya Kati zimeelekea Marekani na Ulaya katika kushindania kwao kuwa na uwezo wa juu zaidi wa kijeshi.
Ripoti hiyo ya taasisi ya Sipri imezitaja Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Uturuki kuwa ndio wanunuzi wakuu wa silaha za Marekani. Saudia ni soko nono la uuzaji silaha za Uingereza pia ambapo karibu nusu ya silaha zote zilizotengenezwa Uingereza zimenunuliwa na Saudia.
Wezeman amebainisha kuwa kutokana na kutokuwepo chombo cha udhibiti silaha katika eneo la Asia, mataifa ya eneo hili yanaendelea kujirundikia silaha na zana za kivita.
Kwa mujibu wa Aude Fleurant, ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi ya Spiri wa mpango wa matumizi ya silaha na zana za kijeshi, Marekani inauza na kusambaza silaha kubwa kubwa kwa nchi zisizopungua 100 duniani, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kulinganisha na wauzaji wengine wa silaha…/

0 comments: