SISITIZO LA WAISLAMU WA NIGERIA LA KUACHILIWA HURU SHEIKH IBRAHIM ZAKZAKY
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 10:26 PM
Wanaharakati wa jumuiya ya kiraia ya Nigeria
wameitaka rasmi serikali ya nchi hiyo imuachilie huru Kiongozi wa
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa
na vyombo vya usalama vya nchi hiyo kwa karibu mwaka mmoja sasa.
Wanaharakati hao wametishia
kwamba, endapo takwa la kisheria la mamilioni ya Waislamu wa Nigeria
halitatekelezwa na serikali na vyombo vya usalama vya nchi hiyo katika
kipindi cha wiki moja ijayo, basi kutafanyika maandamano katika kila
kona ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Katika miezi ya hivi karibuni Waislamu
wengi nchini Nigeria, wakiwa na lengo la kulalamikia marufuku ya
mikusanyiko yao katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyo hususan
Kaduna, wamekuwa wakifanya maandamano ya amani na kukusanyika mbele ya
vituo vya serikali.
Juma lililopita, vyombo vya usalama vya
Nigeria vilibomoa na kuharibu majengo ikiwemo misikiti na shule za
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria katika jimbo la Kaduna, hatua ambayo
ilikabiliwa na malalamiko makubwa ya Waislamu wa nchi hiyo. Uvamizi wa
askari usalama wa Nigeria dhidi ya Waislamu ulikwenda sambamba na
shughuli ya kidini ya Arubaini ya Imam Hussein as.
Waislamu wasiopungua 100 waliuawa shahidi katika shambulio hilo la
jeshi la Nigeria. Ya'kub ambaye ni kaka wa Sheikh Zakzaky anaamini
kwamba, hujuma ya jeshi la Nigeria dhidi ya taasisi za Waislamu katika
jimbo la Kaduna ni njama yenye lengo la kusambaratisha athari za
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Kwa mtazamo huo, baadhi ya mamluki
katika jeshi la Nigeria wana wasiwasi mkubwa kuhusu ushawishi mkubwa wa
harakati hiyo ya Kiislamu katika fikra za waliowengi nchini Nigeria na
barani Afrika kwa ujumla. Maadui wana hofu kubwa ya kuenea dini tukufu
ya Kiislamu na wanaona kuwa, shughuli za Harakati ya Kiislamu ya Nigeria
ambayo iko katika nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika,
zitapelekea kuongezeka wafuasi wa dini hiyo tukufu.
Nyaraka zinaonyesha kuwa, baadhi ya
viongozi wa Nigeria ambao fikra na mitazamo yao inaendana na mitazamo ya
madola ya Magharibi kama Marekani, wameazimia kuchunga maslahi haramu
ya Washington na waitifaki wake barani Afrika. Waitifaki wa Marekani
kama Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel wana matarajio kwamba,
kuongezeka ushawishi na satuwa ya Washington kwa waitifaki wake wa
Afrika kama Nigeria kutawaandalia uwanja mwafaka wa kisiasa watawala wa
Riyadh na Tel Aviv katika nchi za Kiafrika.
Hivi sasa umepita takribani mwaka mmoja tangu Sheikh Ibrahim Zakzaky
alipotiwa mbaroni na kushikiliwa korokoroni huku makundi ya kiraia
nchini Nigeria yakipaza sauti kwa pamoja na Waislamu yakitaka kuachiliwa
huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu. Disemba mwaka jana, jeshi
la Nigeria lilifanya shambulio katika Husseiniyyah ya Baqiyyatullah
katika mji wa Zaria na kuwaua shahidi mamia ya wafuasi wa Sheikh
Zakzaky. Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International
likishirikiana na serikali ya jimbo la Kaduna iliandaa ripoti
yenye kurasa 193 kuhusiana na shambulioa la kinyama la jeshi dhidi ya
Waislamu mjini Zaria. Ripoti hiyo ilifichua kwamba, Waislamu 347
waliuawa kwa umati na kuzikwa katika kaburi la umati. Ripoti hiyo
iliwabainishia Walimwengu ukubwa wa jinai za jeshi la Nigeria dhidi ya
Waislamu hao.
Waislamu wa Nigeria ambao wanaunda
asilimia kubwa ya wakazi milioni 180 wa nchi hiyo, wanataraji kupatiwa
haki zao za kijamii. Takwa hilo bila shaka halionekani kuwa lisilo la
kimantiki hasa kwa kuzingatia hali mbaya waliokuwa nayo Waislamu katika
tawala za kidikteta za chama kimoja au utawala wa kijeshi katika miongo
ya 80 na 90.
Filihali, jumuiya za kutetea haki za
binadamu nazo zinaitaka serikali ya Nigeria imwachilie huru haraka
iwezekanavyo Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye kwa mujibu wa baadhi ya duru,
hali yake ya kiafya hairidhishi tangu jeshi lilipowashambulia Waislamu
mjini Zaria Disemba mwaka jana na kumtia mbaroni kiongozi huyo akiwa
amejeruhiwa vibaya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: