BUNGE LA IRAN LALAANI HATUA YA BUNGE LA MAREKANI

Wajumbe wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, wamelaani hatua ya wajumbe wa Bunge la Marekani kurefusha kwa muda wa miaka 10 sheria ya kuiwekea Iran vikwazo.
Wabunge wa Iran katika kikao cha wazi cha bunge Jumanne ya leo, walitoa taarifa kulaani hatua hiyo ya Marekani na kuitaka serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kukabiliana na uamuzi huo kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Majilisi kuhusu mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Itakumbukwa kuwa, Julai 14 mwaka jana, Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 zilifikia mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Baada ya mapatano hayo Bunge la Iran lilipitisha sheria maalumu ambayo inaainisha ni hatua gani zitakazochukuliwa iwapo moja kati ya madola sita makubwa duniani yatakiuka mapatano hayo.
Bunge la Marekani
Katika taarifa yao, wabunge wa Iran wamesisitiza kuhusu kulinda mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu katika sekta ya nyuklia kwa matumizi ya amani.
Wakati huo huo, Kamal Dehqani Firuzabadi, Naibu Mkuu wa Tume ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Bunge la Iran ameashiria hatua ya Marekani kuvunja ahadi zake na kurefushwa zaidi vikwazo dhidi ya Iran katika Bunge la Marekani, na kusema wabunge watawasilisha muswada wa dharura kuhusu ni hatua gani zichukuliwe kukabiliana na uvunjaji ahadi wa Marekani.
Baada ya ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais, Bunge la Marekani ambalo linadhibitiwa na chama cha Trump cha Republican, lilirefusha kwa muda wa miaka mingine 10 vikwazo dhidi ya Iran sambamba na kupitisha sheria nyingine ya kuzuia Iran kuuziwa ndege.

0 comments: