ULINZI CHUO KIKUU MMH!

CHUO (1)-001
HUKU kumbukumbu za tukio la uvamizi wa kigaidi lililosababisha mauaji ya wanafunzi 147 wa Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya zikiwa bado hazijafifia vichwani, hali ya ulinzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ‘Mlimani’ inasababisha mguno kutokana na watu kupita ndani ya chuo hicho bila ukaguzi.
CHUO (5)-001
Kwa mujibu wa taarifa zilizokifikia kitengo maalum cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ cha Global Publishers, pamoja na chuo hicho kuweka walinzi kwenye mageti yake mawili (Ardhi na Maji), lakini  ukaguzi kwa wenye magari binafsi na ya umma haufanyiki jambo ambalo limetajwa kuwa, kama magaidi wakitokea wanaweza kupenya chuoni hapo.
“Kama unavyojua ulinzi wetu nchini mpaka jambo litokee ndiyo unaimarishwa, ndiyo ilivyo hata pale UDSM. Ukaguzi hakuna, mtu anaweza kuingia na mzigo wowote akiwa kwenye gari binafsi na akapita zake tu getini.(P.T)
CHUO (1)1
“Sasa wewe chukulia ndiyo magaidi wanaingia pale chuo kama wenzetu kule Kenya si itakuwa kazi rahisi sana! Hatuombei itokee lakini wajitahidi kukagua, nyie njooni mjionee ili muwakumbushe wahusika, msiishie huko mitaani,” alisema mwanafunzi mmoja akiomba jina lake lisitajwe.
CHUO (2)-001
Kama ilivyo kawaida, Jumatatu iliyopita, OFM ilitinga chuoni hapo kwa usafiri wake ambapo ilishuhudia magari binafsi na ya umma yakipita getini huku walinzi wakiwa wamesimama na mara kadhaa kuelekeza madereva bila kukagua.
CHUO (3)-001
Hata magari ambayo pengine yangepaswa kutiliwa shaka,  mfano yenye vioo vya giza ‘tinted’ au binafsi ambayo hubeba watu wengi na yale ya mizigo yalikuwa yakipita eneo hilo bila ukaguzi japokuwa kuna kibao nje ya geti kinachosema kwa lugha mbili: TAFADHALI SIMAMA ONYESHA ULICHONACHO/ PLEASE STOP DECLARE YOUR PERSONAL EFFECTS.
CHUO (4)-001
Ili kuthibitisha udhaifu huo, OFM ikiwa na gari lake ilipita mbele ya walinzi hao kuanzia geti la Chuo cha Ardhi mpaka kwenda kutokea upande wa Maji bila kizuizi.
Baada ya hapo, OFM iligeuza kurudi na kwenda Kituo Kidogo cha Polisi Mlimani ili kuzungumza na uongozi kuhusu hali ya ulinzi ambapo ilielezwa mwenye mamlaka ya kusema ni afisa uhusiano wa chuo ambaye hata hivyo, hakuwepo.
Alipotafutwa kwa njia ya simu na kuulizwa kuhusu suala hilo, afisa uhusiano huyo aliyejitaja kwa jina la Walter Rodney Luanda, alisema kwa sasa yupo mkoani Kilimanjaro kwa shughuli za kiofisi hivyo suala hilo atalizungumzia akipata nafasi.
CHUO (6)-001
Hata hivyo, OFM ilizungumza na kiongozi mmoja wa wanafunzi aliyeomba hifadhi ya jina lake na kukiri uwepo wa udhaifu huo lakini alisema usalama chuoni hapo ni mkubwa kwa vile wanafunzi wamepewa elimu ya ulinzi miongoni mwao kwa kuripoti jambo lolote wanalotilia shaka.

0 comments: