Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa udhamini wa kampuni ya Azam Media kupitia Azam tv Sports HD, leo wamezindua kombe la Shirikisho litakalofahamika kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambalo litaanza kutimua vumbi mwezi Novemba mwaka huu kwa kushirikisha timu 64 nchini.
Kurudishwa kwa michuano hii imekua ni faraja kwa wapenzi na wadau wa mpira miguu nchini baada ya kukosekana kwa takribani miaka 13 michuano hiyo, ambapo sasa Bingwa wa kombe la Shirikisho ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAFCC).
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzindizi wa michuano hiyo na kuchezeshwa droo ya awali, Rais wa TFF Jamal Malinzi amemshukuru Mkurugenzi wa Azam Media Rhys Thorrington kwa kuweza kudhamini michuano ambayo itongeza ushindani zaidi nchini.
Malinzi amesema anaviomba vilabu vitakavyoshiriki michuano ya kombe la hilo, vioneshe ushindani mkubwa kwani ndio nafasi pekee ya kuweza kujitangaza na kuonekana kwa kuwa michuano hiyo itakua ikionyeshwa moja moja na luninga ya Azam tv.
Aidha Malinzi amesema kila timu inayoshiriki michuano hiyo itapata fedha ya usafiri shilingi milioni 3, na vifaa vitakavyotolewa na mdhamini kampuni ya Azam Media.
Naye Mkurugenzi wa Azam media Rhys Thorrington amesema udhamaini huo wa miaka mine una thamani ya fedha za kitanzania bilioni 3.3 ambapo timu zitakazoshiriki michuano hiyo zitapata nafasi ya kuonekana moja moja katika nchi zaidi ya saba barani Afrika kupitia kituo chao cha Azam tv.
Mshindi wa Kombe la ASFC linalodhaminiwa na kampuni ya Azam kupitia Azam tv Sports, atajinyakuliwa kitita cha shilingi milioni hamsini (TZS 50,000,000), jumla ya timu 64 kutoka Ligi Kuu (VPL), ligi daraja la kwanza (FDL) na ligi daraja la pili (SDL) zitashirki katika kombe hilo.(P.T)
0 comments: