IDADI YA WATALII YAZIDI KUONGEZEKA PUGU -KAZIMZUMBWI YAFIKIA 21,248-MTEWA

 




Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe

IDADI ya watalii wanaotembelea Msitu wa Hifadhi ya Pugu-Kazimzumbwi, wilayani Kisarawe ,mkoani Pwani imeongezeka na kufikia watalii 21,248 kwa mwaka 2023/2024.


Aidha, mapato yaliyopatikana kutokana na watalii hao ni kiasi cha sh.milioni 222.

Akizungumzia ongezeko la watalii na mapato katika hifadhi hiyo, Meneja Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilayani Kisarawe, Mhifadhi Baraka Mtewa alisema, kwasasa kwa mwezi wanapokea watalii takariban 1,000 .Alieleza, kutokana na kutangaza hifadhi na kufanya maboresho kuvutia watalii kuna asilimia 80 ya watalii wa ndani wanaojitokeza na waliobaki ni watalii toka nje ya nchi.

“Msitu huu wa Hifadhi una mazingira asilia na tunatoa huduma ya utalii ikolojia ambapo kuna vivutio vingi ndani ya Msitu na utalii ,ambao tangu mwaka 2018/2019 tulianza na watalii 533 na sasa kuna ongezeko kubwa lililofikia watalii 21,248”

Vilevile Mtewa alifafanua kwamba, utalii wa ikolojia ni zao jipya la utalii nchini ambao unafanyika katika maeneo yaliyo hifadhiwa vizuri ama kwenye maeneo yaliyotengwa ndani ya misitu kwa ajili ya shughuli za utalii.

Anaelezea, utalii ikolojia ni wa tofauti ambapo haujazoeleka kama utalii mwingine, Huu ni utalii wa mazingira unaomfanya mtu aweze kutulia kwa kuangalia miti, kupata hewa safi “physically” anaweza kupunguza msongo wa mawazo kutokana na utalii huo.

Mtewa alisema, wataendelea kuboresha na kutangaza utalii katika hifadhi hiyo ili kuvutia watalii.

Nae mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti alieleza, msitu wa Pugu -Kazimzumbwi ni eneo lenye utalii wanaendelea kujitangaza na kuvutia watalii .

Magoti alieleza, lengo ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambae amefungua milango ya utalii kwa kuweka mazingira bora ya kuvutia watalii.

Mtembeza watalii kwenye hifadhi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Gift alieleza, Msitu huo upo ndani ya Wilaya ya Kisarawe na unasimamiwa na mhifadhi wa utalii ikolojia ambao ni msitu asilia na kunapatikana bwawa ambalo wanafanya shughuli za kuendesha mitumbwi kwa watalii na utalii wa picha”

Anaelezea, Pugu- Nature Reserve ni sehemu ya utalii ya kipekee ambapo katikati ya milima ya Pugu utakutana na Bwawa la asili (MINAKI DAM) lililozungukwa na uoto mzuri wa asili unaofanya maji yaonekane ya kijani.“Katika bwawa hili wanapatikana viumbe mbalimbali wakiwemo Samaki aina ya perege, kambale na unaweza kufanya michezo ya kuongelea au kuvua samaki (sport -fishing).”

Gift anasema, kwenye msitu huo kuna eneo la mapango ambapo watu wanafanya matambiko ,kila mwisho wa mwaka wanaenda kufanya matambiko kwenye mapango maarufu ‘mzimu wa MAVOGA’ ,kufanya utafiti na wengine wakienda kwa ajili ya kuuomba mizimu hiyo kwa imani ya kufanikiwa”“Pia kuna mlima huu unapanda hadi kilele cha mlima utakutana na mwinuko mkali wa kupandisha utakao kulazimu kutumia kamba kujivuta mdogo mdogo hadi kumaliza mwinuko huu, yaani ni safari ya kuvutia na kusitaajabisha”

Gift anaeleza “Katika hifadhi hii kuna takribani aina 3,000 na zaidi za mimea, ikiwemo mti wa Minaki na Mpugupugu ambao mti huu huwezi kuuona wala kuupata kokote kule Duniani, ambayo ndio asili ya majina ya Minaki na Pugu ambako hifadhi hii inapatikana,:;”Mpugupugu ni mti mrefu wenye umbo kama panga lililojisokota(spiral) hali inayofanya uvutie na kuhamasisha kuutazama.

0 comments: