UN: DOLA MILIONI 900 ZAHITAJIKA KUNUSURU MAISHA YA WASOMALI MILIONI 6
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 10:18 AM
Umoja wa Mataifa umesema unahitajia dola
milioni 900 za Marekani kufikia mwishoni mwa mwaka huu kwa ajili ya
kunusuru maisha ya raia milioni 6 wa Somalia wanaohitajia misaada ya
dharura ya kibinadamu.
Akiongea katika ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa
kuhusu Somalia linalofanyika katika mji mkuu wa Uingereza, London hii
leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema Wasomali
milioni 6 wanahitajia misaada ya kibinadamu haraka iwezekanavyo,
wakiwemo watoto wadogo zaidi ya laki 2 na 75 elfu, wanaosumbuliwa na
utapiamlo na lishe duni.
Amesema watoto wa Kisomali wanakodolewa macho na uhaba wa chakula,
maji sambamba na magonjwa mbalimbali yaliyosababishwa na mazingira
machafu.
Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF iliyowasilishwa
katika kongamano hilo ambalo mwenyeji wake ni Waziri Mkuu wa Uingereza,
Theresa May imesema kuwa, raia milioni 2.9 wa Somalia wataendelea
kuishi katika maeneo yanayokumbwa na ukame na baa la njaa hadi kufikia
Juni mwaka huu, na hali hiyo inatazamiwa kuzidi kuwa mbaya iwapo hatua
za dharura hazitachukuliwa.
Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo ameliambia kongamano hilo
kuwa, atafanya juu chini kuona anatekeleza yale yote aliyoyaahidi katika
kampeni za uchaguzi wa rais, hususan kupambana na maadui watatu wakuu
wa taifa hilo ambao ni ugaidi, njaa na ufisadi.
Kongamano hilo linawaleta pamoja wadau wa kimataifa, Umoja wa Mataifa
na nchi wafadhili ili kujaribu kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo
ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kuiwezesha kufikia malengo yake ya
maendeleo, usalama na kustawisha uchumi kufikia mwaka 2020.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: