NYUMBA ZAIDI YA 200 ZAKUMBWA NA MAFURIKO YA MVUA ZANZIBAR; DKT. MABPODI AWAPA POLE WAATHIRIKA
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 1:00 AM
Naibu katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar Dkt. Abdalla Juma akipokea maelezo kutoka kwa viongozi wa
mtaa akiwemo sheha wa shehia ya Tomondo, Mohamed Omar katika eneo la
Ziwa maboga ambapo zaidi ya nyumba 200 zimeathiriwa na mvua za masika
zinazoendelea kunyesha.
Nyumba mbali mbali zilizoathiriwa na maji ya mvua katika eneo la Tomondo Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.
Nyumba zilizovamiwa na maji katika eneo la Meli nne Makaburini Unguja.
Katibu wa Tawi la CCM Tomondo,
Hassan Kipanga Abdalla akimweleza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
hali ya waakazi wa shehia hiyo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha
hivi sasa.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Dkt.Abdalla Juma Saadala akiwafariji wananchi wa eneo la
Mwanakwerekwe Meli nne, waliopata maafa kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha hivi sasa.
Naibu katibu mkuu wa CCM
Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala akimfariji mmoja wa wananchi
ambaye nyumba yake imeporomoka kutokana na mvua za masika zinazoendelea
kunyesha hivi sasa nchini, uko Fuoni Migombani Zanzibar.
……………………………………..
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
ZAIDI ya Nyumba 300 katika maeneo
mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi zimeathiriwa na Mvua za masika
zinazoendelea kunyesha hivi sasa.
Akizungumza katika mtaa wa ziwa
maboga sheha wa shehia ya Tomondo, Bw. Mohamed Omar Said alisema zaidi
ya nyumba 200 katika eneo hilo zimeathiriwa na mvua kwa kujaa maji na
zingine kuporomoka.
Bw. Said alifafanua kwamba baadhi
ya wakaazi wa eneo hilo wamehama katika makaazi yao na kuomba hifadhi
katika maeneo mengine yaliyokuwa salama, huku idadi ya nyumba
zinazoathiriwa na mvua hizo zikiendelea kuongezeka kadri mvua
zinavyioendelea kunyenyesha.
Mbali na maeneo hayo pia katika
mitaa ya Meli nne, Fuoni janga mizini na Fuoni Migombani kuna nyumba
zaidi ya 100 zimeathiriwa na mvua hizo.
Akizungumza juu ya athari hizo,
Mjumbe wa sheha wa shehia ya kibondeni, Bi. Zuhura Ame alisema hali za
baadhi ya wananchi waliopata maafa hayo sio nzuri hivyo wanahitaji
msaada wa dharura.
Alisema kwamba licha ya viongozi
wa majimbo hasa Wabunge, wawakilishi na madini baadhi yao tayari
wameanza kutoa msaada na wengine ndio wanajipanga kufika kwa ajiri ya
kuwafariji wananchi lakini bado panahitajika nguvu za pamoja baina ya
wananchi, vyama vya kisiasa na serikali ili kuinusuru nchi kuingia
katika maafa makubwa.
Naye Mkaanzi wa Mwanakwerekwe,
Mwajuma Salum aliomba serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara
inayohusika na masuala ya Miundombinu kutoa kipaumbele cha kujenga
madaraja makubwa na yenye viwango katika maeneo mbali mbali nchini ili
kuepusha hasara inayotokana na mvua hizo kila mwaka.
“ Tumesikia juzi tu serikali yetu
imetangaza bajeti ya mwaka inayofikia Trioni moja, hivyo tunaomba kama
inawezekana baadhi ya fedha zitumike katika uimarishaji wa miundombinu
yetu kwani wengi tunateseka kwa sasa, mfano pale Mwanakwerekwe Gari za
Shamba kuja mjini ni tabu kwani pale katika Bwawa la maji hakupitiki.”,
alisema Mwajuma.
Alisema licha ya serikali kufanya
ziara katika maeneo hayo bado baadhi ya wananchi hawana makaazi ya
kuishi hivyo wanaiomba serikali iwapatie misaada ya dharura ili nao
wapate huduma muhimu kwa kipindi hichi kigumu.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” aliwaagiza viongozi wa
Serikali za Mitaa Zanzibar kuacha tabia ya kuruhusu uuzaji wa viwanja
na ujenzi katika maeneo hatarishi hasa mabondeni na sehemu zinazotwaama
maji ili kuepuka athari za mafuriko zinazoweza kusababisha vifo na
uharibifu wa mali.
Maelekezo hayo aliyatoa katika
Mtaa wa Tomondo Ziwa maboga na maeneo mengine wakati katika ziara yake
ya kuwafariji wananchi waliopata athari za mafuriko katika maeneo mbali
mbali ya Zanzibar.
Alisema wananchi wanatakiwa
kujenga utamaduni wa kujilinda dhidi ya maisha yao kwa kuchukua
tahadhari ya kutoishi katika maeneo wanayojua kuwa ni hatari juu ya afya
na maisha yao.
Aliahidi kwamba CCM kwa
kushirikiana na serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kuwasaidia
wananchi waliopata athari hizo kwa Unguja na Pemba.
“ Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi
natoa pole sana kwa wananchi wetu wa Zanzibar kwa Unguja na Pemba
walioathiriwa na mvua hizi zinazoendelea kunyesha hivi sasa, kwa upande
wa CCM tutaendelea kuwa nanyi kwa kutoa msaada wa Ari na Mali ili
kuhakikisha mnarudi katika hali yenu ya kawaida.
Pia nakuombeni wananchi ifikie
wakati na sisi tuisaidie serikali yetu kwa kuepuka kuishi ama kununua
sehemu ambazo tunajua kwamba hazifai kuishi binadamu wakati mvua
zinapoanza kunyesha.”, alisema Dkt. Mabodi na kuongeza kwamba CCM
itaendelea kuwa karibu zaidi na wananchi kwa lengo la kuwapunguzia
changamoto hizo.
Dkt. Mabodi aliishauri serikali
kuchukua hatua za haraka za kurekebisha miundo mbinu ya barabara, maji
na umeme kwa baadhi ya maeneo yaliyokubwa na mafuriko hayo ili wananchi
waendelee kupata huduma muhimu za kijamii.
Aidha alitoa wito kwa wananchi
ambao kwa sasa makaazi yao bado yapo salama kujitolea kwa kuwasaidia
wenzao waliopata maafa huku Chama kwa kushirikiana na serikali
wakitafuta njia mbadala za kusaidia katika maeneo hayo.
Sambamba na hayo aliitaka Mamlaka
ya Maji Zanzibar (ZAWA) kutembelea katika maeneo yaliyopata athari hizo
kwa kugawa dawa za kutibu maji ya kunywa sambamba na kutibu visima
ambavyo maji yake hayo salama kwa lengo la kuwanuru wananchi wasipate
maradhi ya miripuka kwa kipindi hichi cha kuelekea katika Mwezi wa
Ramadhani.
Alisema sululisho la kumaliza
tatizo la maafa hayo yanayotokea kila mwaka ni lazima wananchi waache
kujenga katika mitaro ya kusafirisha maji, hali inayosababisha maji
hayo kukosa njia za kupita na kuwaathiri wananchi wengine wasiokuwa na
hatia.
Naibu Katibu Mkuu huyo, Dkt.
Mabodi katika ziara hiyo amefuatana na uongozi wa Mkoa wa Magharibi na
Wilaya ya Dimani akiongozwa na Mwenyeji wake Mwenyekiti wa Mkoa huo ,
Yussuf Mohamed Yussuf na alitembelea maeneo mbali mbali ya Mkoa wa
Mjini Magharibi mengi yakiwa katika Wilaya ya Maghatibi ‘’B” ambayo ni
Tomondo, Mwanakwerekwe Sokoni, Mwanakwerekwe Meli nne, Fuoni Migombani
na Fuoni Chunga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: