Mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua
zinazoendelea kunyesha katika visiwa vya Zanzibar ambayo ni sehemu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yamesababisha shule zote visiwani humo
kufungwa kwa muda.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Amali Zanzibar amesema kuwa mvua hiyo ambayo pia imekuwa ikinyesha
katika kisiwa cha Unguja na Pemba kwa kipindi cha wiki tatu zilizopita
pia imeharibu barabara na mali ya watu.
Riziki Pembe Juma amesema kuwa baadhi ya
shule zimejaa maji na hivyo kuwa vigumu kwa walimu kufunza mbali na
kuwa wanafunzi wanashindwa kufika shuleni kutokana na mafuriko. Waziri
huyo ameongeza kuwa, uamuzi huo umefikiwa kufuatia pendekezo kutoka kwa
kamati ya kukabiliana na majanga ya Zanzibar ambayo iliishauri serikali
kufunga shule hizo kwa usalama wa wanafunzi.
Hata hivyo amesema kuwa wanafunzi wa kidato cha sita waliokuwa wakifanya mitihani yao ya mwisho wataendelea kufanya hivyo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, watu kadhaa
wanadaiwa kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo. Nyumba nyingi
zimejaa maji yaliyosababisha hasara kubwa.
Aidha makumi ya familia zimebakia bila
makazi baada ya nyumba zao kuathiriwa vibaya na mafuriko hayo. Afisa
mmoja wa masuala ya misaada ya kibinamu kwa waathirika visiwani Zanzibar
amesema watu wengi wanahitaji misaada mbalimbali kutokana na kuathiriwa
mno na mafuriko hayo. Mavazi, misaada ya vyakula, vifaa vya afya na
madawa inasemekana kuwa ndio vitu vinavyohitajika zaidi kwa sasa kwa
ajili ya waathiriwa wa mafuruki hayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: