MAMIA YA WAHIJIRI WAHOFIWA KUFARIKI BAADA YA BOTI KUZAMA KATIKA BAHARI YA MEDITERANIA
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 12:58 AM
Wahajiri zaidi ya 200 wanahofiwa kuwa
wamefariki dunia katika bahari ya Mediterania katika muda wa juma hili,
kulingana na ushahidi uliotolewa na manusura na baada ya maiti kadhaa
ikiwemo mtoto mdogo kuopolewa kwenye ufukwe wa pwani ya Libya.
Manusura
hao waliookolewa na kufikishwa Sicily nchini Italia waliwaeleza walinzi
wa pwani ya nchi hiyo hapo jana kuwa zaidi ya watu 60 wanahofiwa kuwa
wamekufa na viwiliwili vitatu viliopolewa siku ya Jumamosi.
Hata hivyo
baadhi ya manusura waliookolewa na kupelekwa mjini Pozzallo, Italia
wameliambia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR)
kuwa idadi ya wahajiri waliofariki inapindukia 80.
Katika upande mwengine, gadi ya pwani ya Libya imewaokoa wahajiri
saba ambao wamesema walikuwa kwenye boti iliyokuwa imebeba watu 170.
Omar Koko, kamanda wa gadi hiyo katika mji wa Zawiya ulioko magharibi
mwa Libya amesema, kwa mujibu wa manusura hao mlikuwa na watu 170 kwenye
boti hiyo iliyozama kutokana na kufurika watu. Kwa mujibu wa Koko
miongoni mwa watu waliotoweka ni wanawake zaidi ya 30 na watoto tisa.
Mohanad Karina, msemaji wa Shirika la Hilali Nyekundu katika mji wa
Zawiya amesema maiti 11 zimeopolewa kwenye ufukwe ulioko magharibi mwa
mji huo ambazo zote ni za wanawake akiwemo mtoto mwenye umri chini ya
mwaka mmoja.
Walinzi wa pwani za Libya na Italia wametangaza kuwa wahajiri wapatao 7,500 wameokolewa tangu Alkhamisi iliyopita.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi,
mbali na ajali za boti zilizotokea hivi karibuni, zaidi watu 1,150
wamefariki au kutojulikana waliko tangu ulipoanza mwaka huu wakijaribu
kuelekea Italia kutokea Afrika Kaskazini. Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi
alitangaza jana kuwa sababu kuu ya ajali hizo za baharini ni kufurika
abiria kwenye boti zinazotumiwa na wasafirishaji watu kimagendo kuelekea
Ulaya…/
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: