UPINZANI CONGO WATAKA UCHUNGUZI KUHUSU PASIPOTI

Viongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamewataka maafisa wa serikali kuchunguza ripoti ya shirika la habari la Reuters iliyochapishwa wiki iliyopita, ikisema sehemu kubwa ya fedha zinazolipwa na raia kwa ajili ya Pasipoti zinakwenda nje ya nchi. Ripoti hiyo kuhusu mkata uliosainiwa mwaka 2015 baina ya serikali ya Kongo na kampuni ya kibelgiji iitwayo Semlex kutengeneza paspoti za kisasa, inaonyesha kuwa gharama ya paspoti moja ni dola 185 za kimarekani, na kwamba nyingi kati ya fedha hizo huenda katika kampuni ya Semlex na nyingine iliyosajiliwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu ijulikanayo kama LRPS. Aidha, ripoti hiyo inamnukuu mtu mwenye ujuzi kuhusu kampuni la LRPS, akisema kampuni hiyo ni mali ya mtu mwenye uhusiano wa karibu na Rais Joseph Kabila, aitwaye Makie Makolo Wagoi. Serikali ya Kongo na Kampuni ya Semlex hawajatoa majibu yoyote kwa taarifa hizo.

0 comments: