UAMUZI WA MAHAKAMA KUU INDIA DHIDI YA VIONGOZI WA CHAMA TAWALA, KUBOMOLEWA MSIKITI WA BABRI

Mahakama Kuu ya India imetangaza kuwa, viongozi watatu wa ngazi za juu wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) wanapaswa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuharibu Msikiti wa Babri na mauaji ya Waislamu.
Watu hao watatu wanatuhumiwa kwamba, waliwachochea Wahindu wenye misimamo mikali kuharibu Msikiti wa Babri katika mji wa Ayodhya, jimbo la Uttar Pradesh, kaskazini mwa India tarehe 6 Disemba 1992, suala ambalo lilizusha hitilafu na machafuko makubwa ya kikaumu na kusababisha mauaji ya maelfu ya watu. Wahindu wenye misimamo mikali waliharibu msikiti huo kwa lengo la kujenga hekalu la Ram mahala pale.
Majaji wa Mahakama Kuu ya India wamesema, Uma Bharti, waziri wa maji, L K Advani, Naibu Waziri Mkuu wa zamani pamoja na mwanasiasa mashuhuri M M Joshi, wote hao wa chama tawala BJP wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya jinai na kula njama, kwa kuwachochea vijana wenye misimamo mikali wa Kihindu kuubomoa Msikiti wa Babri uliojengwa karne ya 16.
Machafuko yuliyosababishwa na kubomolewa msikiti huo na hitilafu zilizotokea baina ya Waislamu na Wahindu vimesababisha mauaji ya Waislamu zaidi ya elfu mbili na kujeruhiwa wengine wengi.  
Awali mahakama hiyo ilitosheka kwa kumkosoa aliyekuwa mkuu wa chama cha Bharatiya Janata, Subramanian Swamy kwa kufanya njama za kuboa Msikiti wa kihistoria wa Babri na kutaka kujenga maabadi ya Wahindu mahala pale.  Mahakama Kuu ya India ilisisitiza kuwa, chama cha Bharatiya Janata hakiwezi kufikia malengo yake katika jimbo la Uttar Pradesh kwa kutumia mabavu. 
Wahindu wakibomoa Msikiti wa Babri

Rai ya sasa ya Mahakama Kuu ya India inayotaka kupandishwa kizimbani viongozi wa ngazi za juu wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) kwa kuhusuka na kuharibiwa Msikiti wa Babri na mauaji ya maelfu ya Waislamu inaweza kutambuliwa kuwa ni mpambano baina ya serikali na Idara ya Mahakama ya nchi hiyo. Chama cha Bharatiya Janata ambacho kilishika hatamu za uongozi nchini India baada ya kushinda uchaguzi wa Bunge mwaka 2014 - kama ilivyokuwa imetabiriwa- kilizidisha mashinikizo na ukandamizaji dhidi ya Waislamu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Katika mkondo huo huo, kwa wiki kadhaa sasa chama hicho kimekuwa kikishinikiza Mahakama Kuu ya India kwa shabaha ya kuilazimisha itoe hukumu kwa maslahi ya viongozi wake. Hata hivyo hukumu ya mahakama hiyo imekwenda kinyume na matakwa yake.
Waislamu wa India wana wasiwasi mkubwa kuhusu utendaji wa chombo hicho cha sheria na uwezo wake wa kulinda msingi wa kutopendelea upande wowote katika kesi muhimu sana baina ya Wahindu na Waislamu. Vilevile duru mbalimbali za India zinasema kuwa, Wahindu wenye misimamo mikali wangali wanashikilia misimamo yao kuhusu ujenzi wa maabadi ya Ram sehemu ya Msikiti wa kihistoria wa Babri licha ya uamuzi wa mahakama hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mpango wa kujenga maabadi hiyo sehemu ya Msikti wa Babri umekuwa ukitajwa sana katika ahadi za chama tawala cha Bharatiya Janata katika kampeni za uchaguzi. 
Msikiti wa Kihistoria wa Babri

Wahindu wenye misimamo mikali wanadai kuwa, kabla ya kujengwa Msikiti wa Babri kulikuwepo hekalu au maabadi ya Ram mahala hapo, madai ambayo hayana mashiko ya kihistoria.
Hivi sasa baada ya Mahakama Kuu ya India kutoa hukumu ya kupandishwa kizimbani viongozi wakuu watatu wa chama tawala kwa tuhuma za kuhusika na ubomoaji wa Msikiti wa Babri na mauaji ya maelfu ya Waislamu wa India, kuna wasiwasi kwamba chama cha Bharatiya Janata Party (BJP) kitatumia njia mbalimbali za vishawishi na vitisho kwa ajili ya kumshinikiza jaji anayeshughulikia faili hilo ili atoa hukumu dhidi yua Waislamu. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema itakuwa vigumu sana kwa chama hicho kufikia malengo yake baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya India ya kupandishwa kizimbani viongozi hao watatu wa chama cha BJP.

0 comments: