UN YAIONYA SAUDIA DHIDI YA KUSHAMBULIA KWA MABOMU BANDARI YA YEMEN

Umoja wa Mataifa umeutaka muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia usishambulie kwa mabomu bandari ya kistaratejia ya Yemen.
Jamie McGoldrick, Mshirikishi wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen ametahadharisha kuwa, iwapo Bandari ya al-Hudaydah iliyopo katika Bahari Nyekundu itashambuliwa kwa mabomu na Saudia, basi yumkini idadi kubwa ya raia wa Yemen wakatumbukia katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu.
Katika kikao na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Jordan, Amman hii leo, afisa huyo wa UN amefafanua kuwa: "Bandari ya al-Hudayda ni kituo nyeti kwa raia wa Yemen, hatuoni iwapo kuna haja ya eneo hilo la kistaratajia kushambuliwa na muungano wa kijeshi wa Saudia. Muungano huo unafaa kulipa uzito na umuhimu suala la kibinadamu unapokuwa katika kampeni na operesheni zake. Iwapo bandari hiyo itashambuliwa, sisi pamoja na asasi zingine za kufikisha misaada ya kibinadamu hatutaweza kufikisha chakula, dawa na mahitaji mengine ya msingi kwa raia wa Yemen."
Jamie McGoldrick, Mshirikishi wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Bandari ya al-Hudaydah ndiyo bandari muhimu zaidi ya Yemen ambapo karibu asilimia 80 ya shehena za chakula na dawa zinazofikishwa kwa wananchi, hupitishwa kupitia bandari hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, wananchi wa Yemen hapo jana walikusanyika mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a kulaani kufungwa Bandari ya al-Hudaydah sambamba na kukosoa mauaji ya kikatili dhidi ya watu wa taifa hilo, yanayofanywa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, tangu Machi mwaka 2015.

0 comments: