RUSSIA NA CHINA ZATUMA MELI ZAO ZA KIJESHI KARIBU NA ENEO ZILIPO MELI ZA US, KOREA

Russia na China zimetuma meli zao za kijeshi katika eneo zilipo meli za Marekani karibu na pwani ya Korea Kaskazini kwa lengo la kufuatilia nyendo za meli za Marekani katika eneo hilo.
Gazeti la Japan la Yomiuri Shimbun limeandika kuwa, serikali ya Uchina imeomba msaada kwa Russia kwa ajili ya kuzuia kutokea mgogoro wa kivita huko Korea Kaskazini. Kwa mujibu wa gazeti hilo, Beijinga na Moscow zimeamua kutuma meli zao za kivita kwa ajili ya kukusanya taarifa za kiintelijensia kutoka meli za Marekani, ili kuzuia kuongezeka kwa mgogoro baina ya Marekani na Korea Kaskazini.
Moja ya meli za kivita za Marekani zilizotumwa Korea
Wakati huo huo gazeti la Japan News, linaloandikwa kwa lugha ya Kingereza limesema kuwa, meli hizo za Uchina na Russia zitakuwa na kazi ya kutoa indhari na kupiga doria sambamba na kuzidisha ulinzi wa kujitawala anga na bahari ya eneo hilo. Awali Rais Donald Trump wa Marekani alitoa amri ya kutumwa meli tatu za kubeba ndege za kivita za 'USS Carl Vinson' 'Ronald Reagan' na 'USS Nimitz' kwenda pwani ya Korea, hatua ambayo ilitajwa na serikali ya Pyongyang kuwa ni ya kichokozi.
Moja ya meli za kivita za Uchina
Katika hatua nyingine serikali ya Korea Kusini imesisitiza azma yake ya kuweka ngao ya makombora ya Marekani aina ya THAAD katika ardhi yake na kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika suala hilo. Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ilisema Jumatatu ya jana katika kujibu baadhi ya tetesi zilizoashiria kuwa Seoul na Washington zimeamua kusitisha zoezi la uwekaji ngao hiyo,  kwamba habari hizo hazina ukweli wowote.

0 comments: