“Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita dunia imeshuhudia nguvu na maamuzi ya rais wetu mpya akichukua hatua huko Syria na Afghanistan. Korea Kaskazini itafanya vizuri iwapo haitojaribu kupingana na maamuzi ya rais,” Makamu wa Rais Pence amesema.
Makamu wa rais huyo anatembelea Korea Kusini katika mwanzo wa ziara yake ya mataifa manne ya Asia kusisitiza nia ya Marekani thabiti kwa kuendelea kuwasaidia washirika wake katika ongezeko la hali tete inayoendelea kujitokeza katika eneo hilo na kujenga mshikamano wa kimataifa kwa kuongeza shinikizo kwa serikali ya Kim Jong Un kukomesha programu zake zakutengeneza silaha za nyuklia na makombora ya ballistiki.
Umoja usiotetereka
Wakati wa mkutano wa waandishi mjini Seoul Jumatatu alioufanya pamoja na kaimu Rais wa Korea Kusini Hwang Kyoahn, Pence amesisitiza msaada wa Marekani “usiotetereka” katika kulinda mshirika wake wa muda mrefu na kushirikiana naye katika maamuzi yote yanayohusiana na usalama wa eneo hilo.
“Tutaendelea kushauriana kwa karibu na Korea Kusini na uongozi wenu tunapoendelea kufanya maamuzi,” alisema.
Wengi huko Korea Kusini wameendelea kuwa na wasiwasi kwamba Marekani inaweza kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini peke yake kitendo ambacho kinaweza kuliingiza eneo hilo katika vita.
Katika maoni yake kaimu rais wa Korea Kusini amesisitiza ulazima wa kuongeza vikwazo vya uchumi dhidi ya Korea na hakuzungumzia suala la kuchukua hatua za kijeshi.
“Tunakubaliana katika uelewa wa uzito na umuhimu wa tishio la nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini, na kuongeza maradufu juhudi zetu kubadilisha mikakati iliowekwa na Korea Kaskazini kwa kuendelea kuongeza shinikizo la mtandao wa kimataifa juu ya Korea Kaskazini,” amesema Hwang.
Mshauri wa Usalama wa Taifa Marekani
Kadhalika April 16, 2017 Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani H.R. McMaster alionekana kuweka kando tishio lililokuwepo juu ya uwezekano wa Majeshi ya Marekani kufanya mashambulizi dhidi ya Korea Kaskazini, angalau kwa wakati huu.
“Ni wakati mwafaka kwetu kuchukua hatua zote zinazowezekana, bila ya hatua za kijeshi, katika kujaribu kulitatua suala hili kwa njia ya amani,” amesema kwenye kipindi cha “This Week” cha shirika la habari la ABC. “Tunafanya kazi na washirika wetu na wadau wengine na uongozi wa China kuandaa njia mbalimbali mbadala za kukabiliana na suala hili.”
Uongozi wa Trump umeripotiwa kuwa umejikita katika kuweka vikwazo madhubuti vya kiuchumi, kukiwa na uwezekano wa kuhusisha kuzuia mafuta kuingia nchi hiyo, kupiga marufuku shirika la ndege la nchi hiyo kimataifa, kukamata meli za mizigo na kuziadhibu Benki za China zinazofanya biashara na Pyongyang.
Pongezi za Trump kwa China
Makamu wa rais amerudia kueleza pongezi za Trump kwa hatua zaidi ilizochukua China katika ongezeko la vikwazo vya uchumi ukiwemo uamuzi wa kuzirejesha meli za mizigo zilizokuwa zimebeba makaa ya mawe, moja ya biashara ya nje muhimu kwa Korea Kaskazini na pia kufuta safari za ndege kwenda Pyongyang.
Wakati China ikiendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kuweka shinikizo la vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini ilikufikia mazungumzo ya kuondoa silaha za nyuklia, imekuwa ikisita kuchukua hatua kali ambazo zinaweza kusababisha kukosekana amani katika nchi za jirani na kuongeza nguvu za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.
0 comments: