NAIBU SPIKA TULIA AKSON AZINDUA MAFUNZO YA SANAA TASUBA


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Akson akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum ya Vikundi vya ngoma za asili kutoka mkoa mbeya yanayofadhiliwa na Tulia Trust.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Akson, akiimba wimbo na Msanii wa muziki wa Bongo fleva , Nandy pamoja na Mtendaji mkuu wa chuo Cha Sanaa Bagamoyo,Herbert Makoye .
Moja ya kazi za Sanaa zilizochorwa katika chuo cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA)
Mmoja wa Wanafunzi kitengo cha Sanaa za ufundi na uchoraji wakichora picha ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Akson



Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii

TAASISI ya Tulia Trust inayomilikiwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson imewafadhili wanafunzi 27 kwa ajili ya kupata mafunzo ya sanaa.

Taasisi hiyo imewadhamini wanafunzi hao kutoka Mbeya kusoma kwenye chuo cha Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa), kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani.

Wanafunzi hao watapata fursa ya kujifunza sanaa ya maonyesho ya upigaji ngoma za asili, maigizo na utumiaji jukwaa.Akizungumza kwenye uzinduzi wa kuwakabidhi wanafunzi hao chuoni hapo, Dkt. Tulia amesema lengo la kuwafadhili vijana hao ni kutokomeza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Amesema taasisi yake imedhamilia kukuza sanaa kwa vijana nchini ili kutatua tatizo la ajira na kuongeza ufanisi kwenye vipaji vyao walivyokuwa navyo awali.Alisema vijana hao wakipata mafunzo kwenye chuo hicho wataweza kufanya shughuli zao za ngoma za asili kiutaalamu zaidi, hali itakayowaongezea kipato na kuwafungulia fursa nyingi.

Dkt. Tulia alisema zoezi la kuwafadhili vijana kusoma kwenye chuo hicho litakuwa endelevu ili kukuza vipaji vya vijana kwenye sanaa.Alisema baada ya awamu ya kwanza kumalizika atahakikisha anaongeza idadi ya vijana atakaowadhamini kwa ajili ya kukuza vipaji vya sanaa nchini hususani kwenye mkoa wa Mbeya.

Tulia, alisema atahakikisha kwenye awamu ya pili atachukua wanawake wenye vipaji ili kuendeleza vipaji vyao kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

"Huu hautakuwa mwisho wa kufadhili vijana, nitahakikisha naongeza idadi ya vijana kwenye awamu ya pili. Juhudi hizi zitahakikisha zinasaidia vijana wanaepuka tatizo la ukosefu wa ajira nchini," alisema Tulia.

Aidha, Dkt. Tulia amewataka wadau mbalimbali wa sanaa, Taasisi na Kampuni kuunga mkono juhudi za taasisi yake kwa ajili kukuza sanaa nchini.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TaSUBa, Dkt.Herbert Makoye, alisematahakikisha chuo chake kinawapa mafunzo mazuri vijana hao ili kuwaongezea ufanisi kwenye vipaji vyao.

Alisema watahakikisha wanawapa mafunzo mazuri ya uchezaji ngoma za asili, ngoma za ubunifu, muziki wa asili ya Tanzania, uigizaji, matumizi ya jukwaa na maleba.

Dkt Makoye, alisema ana imani vijana hao wakihitimu mafunzo hayo watakuwa tofauti na walivyokuwa hapo awali.

Mafunzo hayo yatadumu kwa kipindi cha miezi miwili watakaofuzu wataendelea na kozi ya cheti na diploma kwa ajili ya kukuza vipaji vyao.
Mtendaji mkuu wa chuo cha Sanaa Bagamoyo(TASUBA) akizungumza kumkaribisha Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Akson
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Akson akiwasili katika chuo cha Sanaa Bagamoyo kwa jili ya ufunguzi wa mafunzo kwa vikundi vya Sanaa mkoa mbeya.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Akson, akicheza ngoma pamoja na Mtendaji mkuu wa Chuo Cha Sanaa Bagamoyo , Dk Herbert Makoye

0 comments: