KAMPALA KUWASTAAFISHA WAKONGWE UPDF WAKIWEMO MAJENERALI
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 1:56 AM
Baada ya kutumikia jeshi la Uganda (UPDF) kwa zaidi ya miaka 36
wanajeshi wote wakongwe wanastaafishwa na nafasi zao kuchukuliwa na
vijana.
Hata hivyo serikali haijatoa sababu maalum ya uamuzi huo wa
kuwastaafisha wanajeshi hao ambao wanajulikana kwa ushujaa wao wa
kupigana vita vilivyomwezesha Rais Yoweri Museveni kuingia madarakani
mwaka 1986.
Lakini kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi hilo Brigedia Richard Karemire hiyo ni hatua ya kawaida.
“Tutakuwa na uwezo wa kuwastaafisha zaidi ya maafisa 2000, wakiwemo majenerali,” amesema msemaji huyo.
Ameongeza kusema kuwa: “Tunalenga kuwastaafisha wanajeshi zaidi ya
2000 wakiwemo majenerali na zaidi ya wanajeshi wengine 10,000
watastaafu.”
“Hii ni sehemu ya zoezi ambalo limekuwa likiendelea kwa miaka mingi.
Tunalenga kuimarisha utendaji kazi wa jeshi letu, kwani huko nyuma
tayari tumewastaafisha baadhi yao,” amesema Brig Karemire.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa baadhi ya
wanajeshi hawa wamekuwa wakitaka kuondoka jeshini bila ya mafanikio.
Ametoa mfano wa Generali David Tinyefuza ambaye tayari amefungua kesi
ilioendelea katika mahakama nchini Uganda kwa muda wa miaka 8 akidai
haki yake ya kustaafu bila ya mafanikio.
Kwa upande mwengine kumekuwa na baadhi ya wachambuzi ambao wamekuwa
na maoni kuwa kulazimishwa kwa wanajeshi hao kubakia jeshini kunatokana
na hofu kwamba wakiruhusiwa kustaafu wanaweza kujiingiza katika siasa na
kuuporomosha utawala wa Museveni.
Mmoja wa wakongwe hao Jeshini Brigedia Generali Kasirye Gwanga
anasema: “ Ni hatua nzuri waruhusu vijana wachukue usukani. Nina umri wa
miaka 65 sasa, nafanya nini katika jeshi, siwezi kukimbia na kushiriki
katika vita.”
Wanajeshi hao wakongwe walishiriki katika vita vya mwaka 1980 na 1985
pamoja na Rais Museveni dhidi ya utawala wake Apolo Milton Obote na
Jenerali Tito Okello na kufanikiwa kumwezesha Museveni kuingia
madarakani mwaka 1986 kwa mtutu wa bunduki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: