TAAARIFA KWA UMMA KUTOKA HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA KUHUSU MOTO UNAOUNGUZA SEHEMU YA MLIMA MERU

post-feature-image
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
Moto mkubwa umezuka mwishoni mwa wiki hii na kuunguza sehemu ya Mlima Meru katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo cha moto huo ni vitendo haramu vya urinaji wa asali ndani ya msitu wa hifadhi hiyo.Wananchi wapatao 200 kutoka vijiji jirani vya Olosinoni na Kisimiri Juu wakishirikiana na TANAPA wamefanikiwa kuudhibiti moto huo ili usiweze kuleta madhara makubwa kwa binadamu hususan wageni wanaotembelea hifadhi kwa lengo la kupanda Mlima Meru.
Hadi sasa hakuna wageni waliodhurika na moto huo na tahadhari zote zimechukuliwa ili kudhibiti madhara zaidi kwa binadamu na shughuli za utalii ndani ya hifadhi.
Shirika la Hifadhi za Taifa linaendelea kuwatahadharisha wananchi juu ya vitendo vya kuingia ndani ya hifadhi bila kibali kwa shughuli ambazo zinaweza kuwa chanzo cha kuzuka kwa mioto hii ambayo husababisha uharibifu wa mazingira pamoja na kuharibu vyanzo vya maji.

Aidha, katika kuhakikisha kuwa moto huo unadhibitiwa kwa haraka, TANAPA imeongeza nguvu kazi ya wananchi wakishirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuweza kuudhibiti moto huo.
Mwisho, taarifa kamili juu madhara yaliyosababishwa na moto huo itatolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuzima moto na umma utaendelea kupewa taarifa ya maendeleo ya zoezi la uzimaji wa moto kila wakati.

Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
21.09.2015
dg@tanzaniaparks.com
www.tanzaniaparks.com
Moto unaoendelea kuwaka Mlima Meru katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Martin Loibooki akiongea na wanakijiji wa Olosinoni wanaoshiriki zoezi la kuzima moto unaonendelea kuwaka Mlima Meru katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha jana.

0 comments: