Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Zimbabwe nchini, Mhe. Helen Bawange Ndingani, Balozi Mteule wa Italia nchini, Mhe. Giuseppe Sean Coppola na Balozi Mteule wa Rwanda nchini, Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaaam tarehe 6 Agosti, 2024.
Akipokea nakala hizo Waziri Kombo amewapongeza mabalozi hao kwa uteuzi waliuopata na pia amewaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi watakachokuwa nchini kuziwakilisha nchi zao.
Aidha, ameeleza Mabalozi hao Wateule wanatarajiwa kuwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 12 na 13 Agosti, 2024.
Akiongea na Balozi Mteule wa Zimbambwe nchini, Mhe. Ndingani, Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania na Zimbabwe zimekuwa na ushirikiano wa kihistoria na kindugu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili Hayati, Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati, Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Vilevile, akamkaribisha Mhe. Ndingani kutembelea Maktaba ya Hayati Mwl. Nyerere iliyopo Butiama, mkoani Mara ambayo imesheheni historia yake.
Balozi Kombo pia, akaeleza umuhimu wa kuwekeza na kurithisha historia ya ukombozi kwa vijana ili waweze kufahamu kwa kina namna waasisi hao walivyojitoa kupigania uhuru wa Bara la Afrika hususan harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.
Viongozi hao pia jadili juu ya umuhimu wa kufanyika kwa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zimbabwe ambapo ameeleza kuwa Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano huo. Tanzania na Zimbabwe zinashirikiana katika masuala ya biashara, uwekezaji, usafirishaji, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi, elimu, Sanaa na utamaduni, na sekta nyingine za kisiasa.
Akizungumza na Balozi Mteule wa Italia nchini, Mhe. Coppola, Mhe. Waziri Kombo amesisitiza kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kuendeleza ushirikiano na nchi hiyo ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kupitia mpango wa ushirikiano wa Italia na Afrika unaofahamika kama “Mattei Plan”. Tanzania na Italia zinashirikiana katika sekta za utalii, elimu, Maji, biashara na uwekezaji, kilimo, mifugo na uvuvi, na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na ngozi ili kukuza biashara yake kimataifa.
Tanzania na Italia zinatarajia kuwa na Kongamano la biashara litakalofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Desemba, 2024 kwa lengo la kukuza sekta ya biashara na za kiuchumi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili amabapo, pembezoni mwa kongamano hilo kutafanyika mashauriano ya kisiasa.
Vilevile, katika mazungumzo yake na Balozi wa Rwanda, Mhe. Jenerali, Patrick Nyamvumba, Mhe. Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Rwanda kupitia ujirani wa nchi hizo mbili sambamba na kusimamia makubaliano mbalimbali yaliyokubaliwa katika nyakati tofauti na majukwaa mbalimbali ambayo nchi hizo mbili zimekubaliana kuyatekeleza.
Tanzania na Rwanda zinashirikiana katika sekta za mawasiliano, biashara na uwekezaji, usafirishaji, elimu, utamaduni na michezo, miundombinu, kilimo na mifugo.
Jukumu hili la kupokea Nakala za Hati za Utambulisho limefanywa na Mhe. Waziri Kombo kwa mara ya kwanza tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
0 comments: