Na Mwandishi wetu, Ngorongoro.
KUNDI LINGINE LENYE WANANCHI 564 LAHAMA HIFADHI YA NGORONGORO.
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 2:23 AMZoezi la wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kujiandikisha na kuhama kwa hiari limepamba moto ambapo leo tarehe 28 Aprili, 2024 jumla ya Kaya 105 zenye wananchi 564 na mifugo 1,540 zimehama katika hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera, Simanjiro, Meatu na Monduli.
Kwa mujibu wa Meneja mradi wa kuhamisha wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari, Afisa Uhifadhi Mkuu Florah Assey, kati ya kaya hizo 105 zenye wananchi 564 wanaohama, kaya 96 zenye watu 520 na mifugo 1,424 zinahamia Kijiji cha Msomera huku kaya 9 zenye watu 44 na mifugo 116 zikihamia wilaya za Simanjiro mkoani Manyara, Meatu Mkoani Simiyu, Monduli mkoani Arusha na Dakawa Mkoani Morogoro.
Assey amebainisha kuwa zoezi la kuelimisha, kuandikisha na kuthaminisha mali za wananchi linaendelea ndani ya hifadhi hiyob ambapo kila kaya inayojiandikisha mkuu wa kaya na wategemezi wake hukabidhiwa nyumba yenye vyumba vitatu katika kiwanja chenye ukubwa wa ekari 2.5, shamba la ekari tano kwa ajili ya kilimo huku maeneo waliyohamia yakiwa na miundomnibu yote muhimu ya kijamii.
Akiaga kundi hilo kwa niaba ya Serikali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Bw. Murtallah sadiki mbillu amewasihi wananchi hao wanapofika Msomera kutoruhusu ndugu waliowaacha Ngorongoro kuhamia Msomera bila kufuata utaratibu wa kiserikali unaohusisha kupata stahiki zao zote kwa mujibu wa sheria.
“Naomba nisisitize kuwa mwananchi hapaswi kuhamia msomera bila utaratibu na kwenda kuishi kwa ndugu kwa nguvu wakati akifuata utaratibu Serikali inampa stahiki zake zote kwa mujibu wa sheria, tumepokea changamoto ya mwananchi aliyehamia Msomera bila utaratibu na alipoona mazingira ni mazuri akavamia kwenye Nyumba iliyojengwa ambayo hajakabidhiwa kwa utaratibu, hivyo ni vizuri kufuata sheria na utaratibu” aliongeza Mbillu.
Amewaasa wananchi hao kuwa inapotokea Changamoto yoyote wanapokuwa Msomera au maeneo mengine wanayohamia kuwasiliana na Viongozi wa Serikali katika maeneo hayo badala ya kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii au baadhi ya Vyombo vya habari.
Mkurugenzi huyo amewahakikishia wananchi wanaohama kuwa Serikali inafanya zoezi hilo kwa lengo na kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwajengea miundombinu wezeshi nje ya hifadhi na kwamba zoezi hilo litaendelea kutekelezwa kwa kuzingatia misingi ya Sheria kanuni, taratibu na haki za binadamu.
Kwa upande wake kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Victoria Shayo ameeleza kuwa kwa sasa vijiji vyote ndani ya hifadhi vimefikiwa na timu za uandikishaji na kufafanua kuwa vitendea kazi ikiwemo Vishkwambi vya kuandikishia zaidi ya 50 na magari vimeongezwa ili kuongeza kasi ya uandikishaji kutokana na wananchi wanaotaka kuhama kuwa mkubwa.
“Nawahakikishia kuwa zoezi hili litaendea kufanyika kwa kasi na kuzingatia ufanisi kwa kuwa timu zetu za uhamasishaji, uandikishaji, tathmini na kuhamisha zina ari na utayari mkubwa na zinajitoa kufanya kazi ili kuisaidia Serikali kuboresha Maisha ya wananchi” alisisitiza kaimu kamishna.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: