WATAALAMU WA UN WALAANI SAUDIA KUBOMOA TURATHI ZA KIUTAMADUNI ZA MJI WA KISHIA

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameulaani utawala wa Saudi Arabia kwa kubomoa turathi za mji wa kale wa Waislamu wa madhehebu ya Shia mashariki mwa nchi hiyo.
Katika taarifa, Karima Bennoune Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za kiutamaduni amesema hatua ya Saudia kubomoa eneo la kale la mji wa Awamyah linalojulikana kama al Masourah ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Amesema watawala wa Saudia wamebomoa turathi hiyo ya kiutamaduni pamoja na kuwa walikuwa wametakiwa na Umoja wa Mataifa kutofanya hivyo.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia Ofisi  ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, Bennoune amesema vikosi vya usalama vya Saudia vimeharibu kabisa majengo ya kihistoria na kuwalazimisha wakaazi kukimbia eneo hilo.
"Uharibifu huu unafuta kabisa historia na turathi ya utamaduni na ni ukiukwaji wa wazi wa majukumu ya Saudia kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu," amesema afisa huyo wa Umoja wa Mataifa,
Vifaru vya Saudia vinatumika kuwahujumu raia wa nchi hiyo
Baadhi ya majengo ya eneo hilo yanaripotiwa kujengwa zaidi ya miaka 400 iliyopita. Kwa upande wake Leilani Farha, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya makazi bora ameonya kuwa hatua hiyo ya Saudia kubomoa makaazi ya kale ya Waislamu wa madhehebu ya Shia inahesabiwa kuwa, 'ufurushaji wa lazima katika sheria za kimataifa za haki za binadamu"
Mnamo Mei 10, watu wawili waliuawa wakati wanajeshi wa Saudia walipovamia eneo la al Masourah na kubomoa nyumba za kale katika eneo hilo.
Watawala wa Saudia wamekiharibu kijiji cha al-Masourah ambako ndiko alikozaliwa Sheikh Nimri Baqir an-Nimr, mwanazuoni mkubwa wa Waislamu wa Kishia aliyeuawa kwa kukatwa kichwa na utawala huo mwaka jana. Watawala hao wa Saudia walikibomoa kijiji hicho kwa madai ya eti kukiboresha.
Kijiji cha al-Masourah kinafahamika kama nembo ya malalamiko huko mashariki mwa Saudia dhidi ya watawala wa nchi hiyo ya kidikteta.

0 comments: