WASIWASI WA UMOJA WA ULAYA KUHUSIANA NA HALI YA BAHRAIN

Umoja wa Ulaya umetoa taarifa ambayo imeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya Bahrain na kutoa indhari kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya imesisitiza juu ya ulazima wa kuandaliwa mazingira ya mazungumzo kwa shabaha ya kupatikana maridhiano ya kitaifa na kutuliza hali ya mambo katika nchi hiyo. Taarifa hiyo imesema bayana kwamba, serikali ya Bahrain ina jukumu kwa raia wake.
Sehemu nyingine ya taarifa ya Umoja wa Ulaya imeeleza waziwazi kwamba, mapigano baina ya vikosi vya usalama na raia katika kitongoji cha Diraz kilichoko kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Manama ambapo ndipo yalipo makazi ya Ayatullah Sheikh Issa Qassim yamezusha wasiwasi mkubwa na kwamba, kuendelea kwa hali hiyo kutaitumbukiza nchi hiyo katika hatua nyingine. 
Ukandamizaji wa vikosi vya usalama vya Bahrain
Umoja wa Ulaya unaonyesha wasiwasi wake kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya ndani ya Bahrain katika hali ambayo, ukweli wa mambo ni kuwa, utawala wa Aal Khalifa unaendelea na siasa zake hizo za ukandamizaji kwa himaya ya wazi ya madola ya Magharibi. Katika miezi ya hivi karibuni, utawala huo umeshadidisha siasa zake za ukandamizaji katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi. Mifano ya wazi ya kushadidi siasa hizo ni kutekelezwa hukumu ya kunyongwa vijana watatu wa Kibahraini katikati ya mwezi Januari na vilevile kuuawa vijana wengine watatu wa nchi hiyo mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu.
Matukio hayo yalilifanya Bunge la Ulaya mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu liutake Umoja wa Ulaya uchukue hatua kali zaidi katika uga wa haki za binadamu hasa kwa kuzingatia ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa  huko Bahrain. Kutotumia nguvu kupita kiasi vikosi vya usalama na viongozi wa nchi kutojichukulia tu maamuzi ya kuwapokonya uraia wananchi wake ni miongoni mwa mambo yaliyokuweko katika azimio la Bunge la Umoja wa Ulaya lililotaka kuzingatiwa na kutekelezwa masuala hayo kikamilifu. Pamoja na hayo si tu kwamba, hakujaonekana mabadiliko yoyote chanya katika hali ya Bahrain, bali  siasa za ukandamizaji zimeshika kasi na kuchukua mkondo mpana zaidi. Hadi sasa watu sita wameuawa shahidi, tangu vikosi vya usalama vya Bahrain vilipoizingira nyumba ya Sheikh Issa Qassim mwanzoni mwa mwezi huu wa Mei. 
Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mashuhuri wa Bahrain 
Licha ya msimamo huo wa Umoja wa Ulaya wa kuukosoa utawala wa Aal Khalifa, swali la kimsingi hapa ni hili kwamba, je,kwa nini Wamagharibi ikiwemo Marekani na madola ya Ulaya yangali yanaendelea kuuunga mkono utawala wa Bahrain?
Katika kipindi chote cha miaka sita tangu lilipoanza vuguvugu la wananchi wa Bahrain mwaka 2011 la kulalamikia ukandamizaji na mbinyo wa watawala wa ukoo wa Aal Khalifa, kutaka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi, madola ya Magharibi zikiwemo nchi za Ulaya zimenyamazia kimya ukandamizaji mkubwa unaofanywa na utawala wa Manama dhidi ya raia wa nchi hiyo. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kimya hicho chenye maana kubwa, kimetoa baraka za kuendelezwa ukandamizaji huo.
Baadhi ya nchi za Ulaya kama Uingereza na Ujerumani zikishirikiana na Marekani zimeendelea na hatua zao za kuuzia silaha utawala wa Bahrain na kwa msingi huo kusaidia hatua za ukandamizaji dhidi ya raia zinazofanywa na utawala wa Aal khalifa. Hivyo basi, taarifa ya hivi karibuni ya Umoja wa Ulaya ya kuonyesha wasiwasi wake kwa hali ya mambo nchini Bahrain unaweza kuwa mfano mwingine wa siasa za kindumakuwili za umoja huo mkabala na ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi nyingine.

0 comments: