RAIS JACOB ZUMA WA AFRIKA KUSINI KUFANYA ZIARA YA KITAIFA YA SIKU TATU NCHINI

Rais wa Afrika Kusini, jacob Zuma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu Ziara ya Rais wa Afrika Kusini nchini Mhe. Jacob Zuma, ambaye atawasili nchini kwa ziara ya siku 3. Pamoja na mambo mengine, Rais Zuma pia atatembelea Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha tiba ya ugonjwa wa moyo (Jakaya Kikwete Cardiac Institute), na pia kufungua rasmi Ubalozi wao hapa nchini. 
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Suleiman Salehe, akimsikiliza Waziri Mahiga (Hayupo pichani) katika mkutano na waandishi wa Habari 
Sehemu ya waandishi wa habari wakinukuu maeneo mbalimbali yaliyotajwa na Waziri Mahiga kwenye mkutano na waandishi wa habari. 
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea. 

Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Afrika Kusini nchini

1. UTANGULIZI

(i) Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Gedleyihlekisa Zuma anatarajiwa kufanya Ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini, kuanzia tarehe 10 hadi12 Mei 2017, kwa mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(ii) Ziara hii inafanyika baada ya Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais Zuma kukutana mjini Addis Ababa, Ethiopia wakati wa Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

(iii) Mheshimiwa Rais Zuma anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 10 Mei 2017, jioni na kupokelewa na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Magufuli. 

(iv) Ziara hii itatoa fursa kwa Viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa pamoja ‎na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara. Ujio wa Mheshimiwa Rais Zuma ni fursa nzuri sana ya kuendelea kukuza na kuimarisha zaidi mahusiano mazuri naya kihistoria kati ya nchi zetu mbili. 

(v) Mheshimiwa Rais Zuma anafuatana pia na wafanyabiashara takribani 80. Hii ni fursa muhimu sana katika kukuza mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Hivyo, tarehe 11 Mei 2017, kutakuwepo na Kongamano la Wafanyabiashara katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere (JINCC).

(vi) Ziara ya Mheshimiwa Rais Zuma inaenda sambamba na vikao vya Tume ya Pamoja ya Marais (Bi-National Commission - BNC) kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Mkutano wa Marais umepangwa kufanyika tarehe 11 Mei, 2017. Mkutano huo utatanguliwa na Kikao cha Mawaziri kitakachofanyika tarehe 10 Mei, 2017 na kikao cha Makatibu Wakuu kitafanyika tarehe 8 na 9 Mei, 2017.
2.0. RATIBA
(i) Wakati wa ziara hiyo, tarehe 11 Mei 2017, Mheshimiwa Rais Zuma atakutana na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Magufuli kwa mazungumzo ya faragha kabla ya kushiriki mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili.

(ii) Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa Mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ya ushirikiano. 

(iii) Siku hiyo hiyo, Mheshimiwa Rais Zuma atashiriki chakula cha mchana na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini katika Hoteli ya Hyatt Regency. Pia, Mheshimiwa Rais Zuma na Mheshimiwa Rais Magufuli watashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini litakalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

(iv) Aidha, jioni ya siku hiyo, Mheshimiwa Rais Zumana ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mheshimiwa Rais Magufuli.

(v) Tarehe 12 Mei 2017, Mheshimiwa Rais Zuma anarajiwa kufungua rasmi Jengo jipya la Ubalozi wa Afrika Kusini nchini pamoja na kutembelea Taasisi ya Matibabu ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

(vi) Mheshimiwa Rais Zuma na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Afrika Kusini.


3.0. MAHUSIANO BAINA YA TANZANIA‎ NA AFRIKA KUSINI

(i) Mahusiano ya Tanzania na Afrika Kusini ni mazuri na ni ya muda mrefu tangu wakati wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini zilizoongozwa na Chama kikongwe cha African National Congress (ANC). Nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kikanda na hasa ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Kwa sasa, Afrika Kusini ni Mwenyekiti wa SADC na Tanzania ni Mweyekiti wa SADC Organ, hatua inayotoa nafasi ya kushirikiana zaidi. 

(ii) Aidha, ushirikiano baina ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa ukiimarika kila mara kwa Viongozi wakuu kutembeleana na viongozi wa ngazi za juu Serikalini kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi zetu mbili. Kama mtakumbuka Julai 2011, Mhe. Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alifanya Ziara ya Kiserikali nchini Afrika Kusini ambayo ndiyo iliyozaa Mkataba wa Ushirikiano wa Tume ya Marais ambayo ndiyo iliyotuwezesha kukutana leo.

(iii) Uhusiano wa Vyama vya Siasa vya CCM na ANC

Vyama vya ANC na CCM vina mahusiano mazuri na Viongozi wa vyama hivyo wamekuwa wakikutana mara kwa mara kwa ajili ya kujadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati yao.

(iv) Mikataba ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini

Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hadi sasa, Tanzania na Afrika Kusini tayari zimetia saini Mikataba ya Ushirikiano (MoU) kumi na tano (15), ambayo inagusa sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, sayansi na teknolojia, uwekezaji, utamaduni na kilimo.

(v) Ushirikiani katika Utatuzi wa Migogoro katika Kanda

Tanzania na Afrika Kusini zimeendelea kufanya kazi pamoja katika juhudi za utatuzi wa migogoro na kuhakikisha kwamba Afrika inakuwa sehemu salama. Nchi hizi mbili zimeshiriki katika kutatua migogoro nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Sudan Kusini. Tanzania na Afrika Kusini zote zimechangia Askari katika Brigedi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Amani na Usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (United Nation Force Intervention Brigade-FIB) kwa lengo la kutuliza uvunjifu wa amani Mashariki mwa Kongo. Vile vile, nchi hizi mbili kwa pamoja zimekua zikishirikiana katika kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Sudan Kusini.

(vi) Uhusiano katika Nyanja za Uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini

Ø Uhusiano ya uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa ukiimarika siku hadi siku. Uhusiano huo mzuri umezidi kuchochea na kurutubisha ushirikiano wetu wa muda mrefu na wa kihistoria. 

Ø Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zinazochangia idadi kubwa ya wawekezaji wa kigeni nchini Tanzania. Takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Centre-TIC) kimesajili jumla ya miradi 226 kati ya mwaka 1990 hadi 2016. Miradi hiyo ina thamani ya Dola za Kimarekani zipatazo Milioni 803.15 na imetoa ajira zipatazo 20,916.

(vii) Uhusiano katika Sekta ya Biashara

Ø Kiwango cha biashara (volume of trade) imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Mwaka 2007 ilikuwa Tsh Milioni 976,331 na mwaka 2016 ni Tsh 2,402,211.20. Hili ni ongezeko kubwa na linaleta matumaini ya ushirikiano zaidi.

Ø Bidhaa ambazo Tanzania inauza nchini Afrika Kusini ni pamoja na maua, kahawa, wanyama hai, chai, nguo, pamba, vito vya thamani, tumbaku na mafuta ya kupikia. Bidhaa zinazoagizwa kutoka Afrika Kusini ni pamoja na maziwa na mazao yote ya maziwa, matunda aina ya apple, mbegu za mahindi, mafuta ya soya, sukari kwa matumizi ya viwanda, juisi za matunda, mafuta ya kulainisha mitambo, bidhaa za vileo, Acrylic polymers, lami, magari, pampu za maji, bidhaa za chuma, vitabu, mashine, na trela.

(vii) Mchango wa Madawati wa Afrika Kusini kwa Serikali ya Tanzania

Ø Katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutatua changamoto mbalimbali za kijamii, kwa kupitia Ubalozi wake hapa nchini, Serikali ya Afrika Kusini iliweza kuchangia jumla ya madawati 1100 kwa shule za Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma. Madawati hayo yalikabidhiwa kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI.

Ø Pamoja na hayo, Serikali ya Afrika Kusini inatarajia kuanzisha programu mahsusi ya kubadilishana walimu na uzoefu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuinua sekta ya elimu. 

4.0. TAARIFA FUPI KUHUSU TUME YA USHIRIKIANO YA MARAIS (BI-NATIONAL COMMISSION) KATI YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI

Sasa naomba niwape taarifa fupi kuhusu Mkutano wa Tume ya Ushirikiano ya Marais

(i) Tanzania na Afrika Kusini zilisaini Mkataba wa kuanzishwa kwa Tume ya Ushirikiano ya Marais (Bi-National Commission-BNC) tarehe 19 Julai 2011 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi. Tume ya Ushirikiano ya Marais imechukua nafasi ya Tume ya Uchumi ya Pamoja ya Marais (Presidential Economic Commission-PEC) iliyoanzishwa mwaka 2005. Kama nilivyosema awali, Mkataba huu ulisainiwa wakati wa ziara ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tano, Mhshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

(ii) Mkataba wa kuanzisha BNC umeainisha maeneo kumi (10) ya ushirikiano ambayo ni Biashara na Uwekezaji (Trade and Investment), Maendeleo ya Miundombinu (Infrastructure Development), Kilimo (Agriculture), Elimu, Sayansi na Teknolojia (Education, Science and Technology), Ulinzi na Usalama (Defence and Security), Habari, Utamaduni na Michezo (Infrastructire, Culture and Sports), Afya (Health), Nishati na Madini (Energy and Minerals) na Maliasili na Utalii (Natural Resources and Tourism).

(iii) Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Mashirikiano ya Marais (BNC) unatarajiwa kufanyika kuanzia leo, tarehe 8 hadi 11 Mei, 2017. Mkutano wa Marais utatanguliwa na vikao vya Makatibu Wakuu tarehe 8 na 9 Mei, 2017 ukifuatiwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 10 Mei, 2017. Mkutano wa Marais utafanyika tarehe 11 Mei, 2017 ambapo Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais Zuma watakuwa Wenyeviti Wenza wa Mkutano huo. 

(iv) Wakati wa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Marais, Mikataba ifuatayo inatarajiwa kutiwa saini:-

(a) Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Masuala ya Bio Anuwai na Uhifadhi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini (Memorandum of Understanding between the Government of the United Republic of Tanzania and the Government of the Republic of South Africa on Cooperation in the Field of Biodiversity Conservation and Management);

(b)Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Maji kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini; na

(c) Hati ya Makubaliano katika Sekta ya Uchukuzi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini;

(v) Pia kuna Mikataba mingine inaendelewa kufanyiwa kazi na mara itakapokamilika, Mawaziri wa sekta husika watasaini. Mikataba hiyo ni pamoja na wa Sekta ya Utalii, Sekta ya habari, Sekta ya kilimo, sekta ya afya, niitaje hiyo tu kwa sasa.

(vi) Tofauti na Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (BNC) inashirikisha Marais wa Nchi mbili ambapo katika JPC inaishia katika ngazi ya Mawaziri. Ushiriki wa Marais katika Tume ya Pamoja ya Ushirikiano unatoa uzito wa pekee katika utekelezaji wa maeneo ya mashirikiano yaliyoafikiwa.


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Dar es Salaam, 08 Mei, 2017

0 comments: